MEXICO

Jeshi lafanikiwa kumkamata kiongozi wa kundi la Zetas Miguel Trevino

Miguel Trevino mmoja wa viongozi wa kundi la Zetas aliyekuwa anasakwa na Serikali ya Mexico
Miguel Trevino mmoja wa viongozi wa kundi la Zetas aliyekuwa anasakwa na Serikali ya Mexico Reuters

Jeshi la wanamaji nchini Mexico limesema kuwa limefanikiwa kumkamata kiongozi wa juu wa kundi la Zetas linalojihusisha na uuzaji wa dawa za kulevya nchini humo, Miguel Angel Trevino.

Matangazo ya kibiashara

Jeshi limesema kuwa wamefanikiwa kumkamata Trevino wakati akisafiri na wenzake kwenye mji wa Nuevo Laredo na kwamba hawakurushiana risasi kinyume na ilivyozoeleka kwa viongozi kama hao kuwa na silaha muda wote.

Taarifa ya jeshi imeongeza kuwa, mbali na kumkamata Trevino pia wamefanikiwa kukamata kiasi cha dola milioni 2 zikiwa kwenye gari pamoja na silaha nyingien za kijeshi zinazotumiwa na makundi hayo kufanya uhalifu.

Msemaji wa wizara ya mambo ya ndani wa Mexico, Eduardo Sanchez amesema kuwa kukamatwa kwa kiongozi huyo ni hatua muhimu katika harakati za serikali kukabiliana na makundi ya uuzaji dawa za kulevya nchini humo.

Trevino anatuhumiwa kutekeleza vitendo vya uhalifu, mauaji, usafirishaji wa dawa za kulevya, unyanyasaji na biashara haramu ya fedha.

Kundi la Zetas linatajwa kama moja ya makundi hatari ya uuzaji dawa za kulevya nchini Mexico na limekuwa likifanya uasi kwenye miji mbalimbali nchini humo ikiwemo kuwaua polisi walioko mstari wa mbele kukabiliana na bishara haramu ya dawa za kulevya.