NIGERIA-SUDAN-ICC

Mahakama ya ICC yasikitishwa na Serikali ya Nigeria kushindwa kumkamata al-Bashir licha ya kuombwa kufanya hivyo

Rais Omar al-Bashir akitoka nje ya moja ya hoteli aliyofikia mjini Abuja, Nigeria
Rais Omar al-Bashir akitoka nje ya moja ya hoteli aliyofikia mjini Abuja, Nigeria REUTERS/Afolabi Sotunde

Rais wa Sudan Omar al-Bashir ameondoka nchini Nigeria huku mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ya ICC ikitoa hati ya kukamatwa kwa kiongozi huyo lakini maofisa wa Serikali ya Sudan wamekanusha kiongozi wao kuondoka kwa kuhofia kukamatwa.

Matangazo ya kibiashara

Suala la kiongozi huyo kuwepo nchini Nigeria lilizua hisia kali toka kwa wanaharakati wa haki za binadamu ambao walikuwa wanaishinikiza Serikali kumkamata kiongozi huyo anasakwa na mahakama ya ICC kwa makosa ya uhalifu wa kivita alioufanya nchini mwake.

Ofisi ya mwendesha mashtaka wa mahakama ya ICC ilitoa taarifa kudhibitisha kuwa iliiandikia barua Serikali ya Nigeria kutaka vyombo vya usalama kumkamata kiongozi huyo na kumfikisha kwenye mahakama ya ICC.

Hapo jana Serikali ya Nigeria kupitia ikulu ya rais Goodluck Jonathan ilisema haiwezi kumkamata kiongozi huyo kwakuwa hakuja nchini humo kwa mwaliko wa Serikali bali alienda kwa mwaliko wa Umoja wa Afrika ambao walikuwa wameandaa mkutano wa afya kwa viongozi wa bara la Afrika.

hatua ya Nigeria kushindwa kumkamata kiongozi huyo imekosolewa vikali na wanaharakati wa haki za binadamu pamoja na wanasheria ambao wanadai kuwa Nigeria kama moja ya mataifa yaliyotia saini mkataba wa kutambua mahakama hiyo ilikuwa na wajibu wa kumkamata.

Mwaka 2009 na 2010 mahakama ya ICC ilitoa hati ya kimataifa ya kukamatwa kwa rais Bashir na viongozi wengine wa Sudan kwa makosa ya uhalifu wa kivita dhidi ya binadamu uliofanyika kwenye jimbo la Darfur.