KENYA-ICC

Mawakili wa makamu wa rais wa Kenya wapata pigo, majaji ICC waamuru kesi yake kusikilizwa Hague

Mawakili wa naibu wa rais wa Kenya, William Ruto wakiteta na mteja wao wakati wa moja ya vikao vya mahakam hiyo
Mawakili wa naibu wa rais wa Kenya, William Ruto wakiteta na mteja wao wakati wa moja ya vikao vya mahakam hiyo Reuters/Lex van Lieshout/Pool

Mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ya ICC yenye makao yake makuu mjini The Hague Uholanzi imetupilia mbali ombi la mawakili wa makamu wa rais wa Kenya, William Ruto na Joshua Arap Sang kutaka kesi zao zisikilizwe nchini Kenya ama Tanzania.

Matangazo ya kibiashara

Kwenye taarifa iliyosomwa na karani wa mahakama hiyo, imesema kuwa majaji wanaosikiliza kesi hiyo wamezingatia maelezo ya pande zote mbili ya upande wa mashtaka na ule wa utetezi na kuamua kwamba kesi ya Ruto itasikilizwa kwenye mahakama hiyo.

Naibu wa rais, William Ruto anakabiliwa na makosa matatu kwenye mahakam hiyo ikiwemo ya uhalifu dhidi ya binadamu pamoja na uchochezi kufuatia vurugu za mara baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 na kusababisha vifo vya watu zaidi ya elfu 1 na 100 huku wengine laki 6 wakiachwa hawana makazi.

Mwezi uliopita mahakama hiyo ilitangaza tarehe 10 ya mwezi September mwaka huu kuwa ndio tarehe rasmi ya kuanza kusikilizwa kwa kesi dhidi ya Ruto na mwandishi wa habari Joshua Arap Sang.

Uamuzi wa majaji hao umeonekana kuwa pigo kwa mawakili wa Ruto na Sang ambao mwezi January mwaka huu waliiomba mahakama hiyo ikubali kusikiliza baadhi ya kesi nchini Kenya ama Tanzania na pia kupitia njia ya video.

Maelezo ya majaji hao yanasema kuwa kusikiliza kesi hizo nchini Tanzania ama Kenya kutasababisha hali tete kwa ndugu na familia ambazo zilipoteza wenzao wakati wa vurugu hizo na huenda kukatokea vurugu zaidi.

Kwa mantiki hiyo ni wazi pia hata kesi dhidi ya rais Uhuru Kenyatta ikaamuliwa kusikilizwa mjini The Hague na sio Kenya ama Tanzania kama mawakili wake nao walivyoomba.