MISRI-MAREKANI

Polisi nchini Misri wakabiliana na wafuasi wa Morsi usiku wa kuamkia leo

Waandamanaji nchini Misri wakikabiliana kwenye daraja la October usiku wa kuamkia leo
Waandamanaji nchini Misri wakikabiliana kwenye daraja la October usiku wa kuamkia leo Reuters

Maelfu ya wafuasi wa rais aliyeondolewa madarakani nchini Misri, Mohamed Morsi, wamekabiliana na polisi kwenye miji mbalimbali nchini humo, safari hii wakishinikiza kiongozi wao aachiwe huru. Maandamano hayo yanafanyika wakati huu ambapo mjumbe wa Marekani kwa nchi ya Misri, Bill Burns yuko nchini humo kwa mkutano na viongozi wa Serikali ya mpito kuangalia namna ya kumaliza mzozo wa kisiasa nchini Misri. 

Matangazo ya kibiashara

Punde baada ya kuwasili, Burns alitoa wito kwa waziri mkuu Hazem al-Beblawi na mkuu wa majeshi Abdel Fattah al-Sisi kuhakikisha jeshi halijihusishi na siasa wala kuwakamata viongozi wa vyama vya siasa kwa shinikizo la kisiasa.

Burns ametoa wito huo kufuatia kuendelea kushikiliwa kwa viongozi wengi wa chama cha Muslim Brotherhood ambapo ameiomba Serikali kuwaachilia huru viongozi hao akiwemo rais aliyeoondolewa madarakani, Mohamed Morsi.

Marekani inaonekana kutotaka kujihusisha moja kwa moja na mzozo wa Misri ingawa iko mstari wa mbele katika kutaka kitafuta suluhu ya kisiasa nchini humo.

Usiku kucha waandamanaji wamekabiliana na polisi ambao walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wafuasi wa Morsi ambao walikuwa wamezungunga makao makuu ya jeshi.

Licha ya juhudi ambazo zimeendelea kufanywa na jeshi la nchi hiyo kutaka kuelata maridhiano, chama cha Muslim Brotherhood kimekataa kujihusisha na Serikali ya mpito kwa kile viongozi wake wanadai wanamtambua Mohamed Morsi kama kiongozi wao.