URUSI-MAREKANI-SNOWDEN

Snowden aomba kupatiwa hifadhi ya muda nchini Urusi: Wakili

Edward Snowden aliyekuwa afisa usalama na mhandisi wa mtandao nchini Marekani
Edward Snowden aliyekuwa afisa usalama na mhandisi wa mtandao nchini Marekani Reuters

Afisa usalama wa zamani wa Marekani, Edward Snowden anayesakwa na nchi yake hatimaye ametuma maombi ya muda ya kupatiwa hifadhi na Serikali ya Urusi, wakili wake amedhibitisha. 

Matangazo ya kibiashara

Wakili wa Serikali ambaye pia alihudhuria mkutano wa juma lililopita ulioitishwa na Snowden, Anatoly Kucherena amesema kuwa mhandisi huyo ameomba hifadhi ya muda nchini Urusi wakati akifikiria nchi ambayo atakwenda baadae.

Wakili huyo ameongeza kuwa alimwacha Snowden na maofisa wa uhamiaji wa Urusi kwa mahojiano kabla ya kuamua iwapo wampatie hifadhi au la, licha ya kwamba Urusi ilismea iko tayari kufanya hivyo iwapo ataachana na harakati za kisiasa.

Snowden amekuwa akiituhumu Serikali ya Marekani kwa kuendelea kumuwekea vizingiti asifike kwenye nchi ambazo zimekubali kumpa hifadhi na kwamba nchi hiyo inafanya kila linalowezekana kuhakikisha hasafiri nje ya Urusi.

Kauli ya Snowden kwa mara nyingine hapo jana imeongezewa nguvu na rais wa Urusi, Vladmir Putin ambaye amesema anashangazwa na Serikali ya Marekani kutaka kumzua Snowden asifike kwenye mataifa yaliyompa hifadhi.

Nchi nyingi za Amerika Kusini zimesema ziko tayari kumpatia hifadhi Snowden ikiwe Venezuela, Ecuador, Cuba na Nicaragua.

Mpaka sasa Edward Snowden yuko kwenye uwanja wa ndege wa Urusi wa Sheremetyevo akisubiri majibu ya kuomba kupatiwa hifadhi.