UGIRIKI

Wafanyakazi nchini Ugiriki wafanya mgomo wa nchi nzima kupinga mpango mpya wa ubanaji matumizi uliotangazwa na Serikali

Polisi wa Ugiriki wakishiriki kwenye moja ya maandamano nchini humo
Polisi wa Ugiriki wakishiriki kwenye moja ya maandamano nchini humo Reuters

Maelfu ya wafanyakazi nchini Ugiriki hii leo wameshiriki mgomo wa nchi nzima ulioitishwa na shirikisho la wafanyakazi nchini humo kupinga hatua mpya za kubana matumizi zilizotangazwa na Serikali.

Matangazo ya kibiashara

JUma hili Serikali ya Ugiriki ilitangaza mkakati mpya wa ubanaji wa matumizi, mkakati unaolenga kubana matumizi ili kupatiwa mkopo wa fedha toka Umoja wa Ulaya na Shirika la Fedha duniani yakiwa ni masharti mapya.

Maandamano makubwa yameshuhudiwa kwenye mji wa Athens na Thessaloniki ambapo waandamanaji walibeba mabango yenye ujumbe mbalimbali kuishutumu Serikali kuendelea kuwabana wananchi.

Mpango huo wa Serikali utashuhudia kupunguzwa kwa mishahara ya askari wa Umma na wafanyakazi wengine watapoteza ajira zao.

Mamia ya wananchi wengi wao wakiwa ni vijana wamelalamikia hatua hiyo ya Serikali kwa madai kuwa itasababisha maelfu ya vijana kuendelea kukosa kazi kwakuwa wengi watapoteza ajira walizokuwa nazo sasa.

Mswada huu mpya ambao umeanza kujadiliwa na wabunge unatarajiwa kupigiwa kura siku ya Jumatano ambapo iwapo utapitishwa utashuhudia nchi hiyo ikipatiwa mkopo mwingine wa kiasi cha Euro bilioni 6.8.

Takwimu za hivi karibuni nchini Ugiriki zimeonesha tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana limefikia asilimia 64.