MISRI

Watu 7 wapoteza maisha, 410 wanashikiliwa na polisi nchini Misri kufuatia maandamano ya usiku wa Jumatatu

Wafuasi wa Muslim Brotherhood wakikabiliana na polisi mjini Cairo
Wafuasi wa Muslim Brotherhood wakikabiliana na polisi mjini Cairo Reuters

Maofisa wa afya nchini Misri wamedhibitisha kuuawa kwa watu saba na wengine zaidi ya mia mbili wamejeruhiwa kufuatia maandamano ya usiku wa kuamkia leo kati ya wafuasi wa Mohamed Morsi na askari.Vurugu hizo ambazo zilianza jana jioni mara baada ya Futari zilishuhudia maelfu ya wafuasi wa kiongozi huyo wakivamia daraja la October na makao makuu ya jeshi wakitumia mawe na vyuma kuziba barabara.

Matangazo ya kibiashara

Mjini Cairo wanajeshi na polisi walikuwa na kazi ya ziada kuwazuia wafuasi wa Morsi kukabiliana na wafuasi wanaounga mkono mapinduzi yaliyofanyika nchini humo ambao wote kwa pamoja wameapa kukabiliana popote.

Taarifa ya jeshi iliyotolewa hii leo na msemaji wake inasema kuwa zaidi ya watu mia nne wanashikiliwa na polisi wengi wao wakiwa ni wafuasi wa chama cha Muslim Brotherhood ambao ndio walioanzisha vuruguzu za usiku wa kuamkia leo.

Katika hatua nyingine msemaji wa Serikali amedhibitisha baadhi ya viongozi wa Muslim Brotherhood kupewa nafasi kwenye baraza jipya la mawaziri lakini wengi wamekataa kujumuishwa kwenye Serikali ya mpito.

Maandamano ya kuamkia usiku wa leo yalikuwa ni yakushinikiza kuachiliwa huru kwa Mohamed Morsi na maofisa wengine wa Muslim Brotherhood.

Vurugu hizi zinazuka ikiwa imepita wiki moja toka nchi hiyo ishuhudie utulivu kati ya wafuasi wa Morsi na wale wanaounga mkono Serikali ya mpito.