SYRIA-UN

Idadi ya raia wanaokimbia machafuko nchini Syria haijawahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 20: UN

Moja ya kambi ya wakimbizi wa Syria iliyoko nchini Uturuki
Moja ya kambi ya wakimbizi wa Syria iliyoko nchini Uturuki Reuters

Umoja wa Mataifa UN unasema kuwa idadi ya wakimbizi toka nchini Syria wanaokimbia machafuko ya kisiasa imevunja rekodi ya dunia na kuzidi hata wale waliokimbia vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Rwanda mwaka 1994. 

Matangazo ya kibiashara

Kwa mujibu wa ripoti hiyo mpya ya Umoja wa Mataifa, inakadiria kuwa zaidi ya raia elfu sita hukimbia toka nchin humo kila siku na kufanya idadi hiyo kuwa kubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa duniani.

Mkuu wa tume ya Umoja wa Mataifa anaehusika na wakimbizi, Antonio Guterres amesema kuwa ongezeko hili kubwa la wakimbizi halijawahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka ishirini toka kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Rwanda.

Guterres ameyasema hayo wakati wakiwahutubia wajumbe wa baraza la usalama ambapo mbali na kueleza hali ya wakimbizi ilivyo nchini Syria, pia amesema zaidi ya watu elfu tano huuawa kila siku kutokana na mapigano yanayoendelea kushuhudiwa nchini humo.

Kwa upande wake mkuu wa tume ya Umoja hu anaehusika na misaada ya kibinadamu, Valerie Amos amewaambia wajumbe wa baraza la usalama kuwa, zaidi ya watu milioni 6.8 wanahitaji haraka misaada wa kibinadamu.

Ripoti hiyo inatolewa wakati huu ambapo kuna mgawanyiko mkubwa ndani ya baraza la usalama kutokana na baadhi ya nchi ikiwemo China na Urusi kupinga maazimio yoyote ambayo yanataka kuchukuliwa dhidi ya utawala wa rais Bashar al-Assad.

Serikali ya Urusi na China zenyewe zimekuwa zikiutetea utawala wa Syria huku wakipinga kutumika kwa nguvu za kijeshi kuung'oa utawala wa rais Assad.

Marekani na washirika wake wanataka rais Assad aondolewe kwa nguvu madarakani huku wakitangaza hadharani kushirikiana na waasi wa jeshi huru la Syria kwa kuwapatia silaha.

Vita nchini Syria imeendelea kuwa ngumu kutokana na waasi wenyewe kugawanyika huku Serikali ya rais Assad ikisaidiwa na wapiganaji wa Hezbollah wa nchini Lebanon kuwakabilinwaasi kwenye miji ambayo wanaishikilia.