KENYA-WAALIMU

Chama cha waalimu nchini Kenya, KNUT chatangaza kumaliza mgomo huku wizara ya elimu ikitangaza kufunga shule zote za umma

Baadhi ya waalimu wakiandamana nje ya ukumbi wa bunge kushinikiza kulipwa marupurupu yao na Serikali
Baadhi ya waalimu wakiandamana nje ya ukumbi wa bunge kushinikiza kulipwa marupurupu yao na Serikali Reuters

Chama cha waalimu nchini Kenya, KNUT hapo kimetangaza kusitisha mgomo wake wa saa ishirini na nne uliodumu kwa majuma manne baada ya kufikia muafaka na Serikali ambayo walikuwa wanashinikiza kulipwa malimbikizo yao. 

Matangazo ya kibiashara

Walimu hao sasa watarejea kazini wakiwa wameahidiwa kulipwa kiasi cha shilingi za Kenya bilioni 16.2 ikiwa ni fedha za usafiri, uwajibikaji na muda wa nyongeza kama walivyokubaliana na Serikali kwenye mazungumzo ya faragha na naibu rais wa Kenya, William Ruto.

Kusitishwa kwa mgomo huo wa KNUT kunakuja wakati huu ambapo waziri mwenye dhamana na elimu akitangaza kuzifunga shule zote za umma kutokana na shule hizo kukosa walimu mpaka pale itakapoajiri walimu wapya.

Fedha hizo zitalipwa kwa awamu mbili ambapo shilingi bilioni 5.7 zitawekwa kwenye akaunti za walimu hao mapema zaidi huku kiasi kilichobakia kikitarajiwa kumaliziwa kwenye mwaka wa fedha ujao.

Kwa mantiki hiyo sasa waalimu nchini Kenya kulingana na nyadhifa zao watakuwa wakipokea shilingi za Kenya, 4000 hadi 16000 kama fedha za usafiri kila mwezi.

Makubaliano haya pia yanamaanisha kuwa tume ya kuajiri waalimu nchini Kenya, TSC itatakiwa kuwalipa walimu hao mshahara wao wa mwezi June licha ya kuwa kwa muda wote walikuwa nje ya vituo vyao.

TSC pia italazimika kuondoa kesi yake iliyokuwa kwenye mahakama ya viwanda ambapo tume hiyo iliwashtaki viongozi wa KNUT, mwenyekiti wake Wilson Sossion na katibu wake kwa madai ya kukiuka amri halali ya mahakama iliyowataka kusitisha mgomo wao.

Mwenyekiti wa KNUT, Wilson Sossion amesema kuwa baada ya kutafakari kwa kina ofa waliopewa na Serikali wamekubaliana njia muafaka ambazo zitatumika kudai haki yao iliyobako na kwamba baraza kuu la KNUT linamwagiza katibu mkuu kutangaza kusitishwa kwa mgomo huo.

Awali waziri wa elimu, Jacob Kaimenyi alotangaza kufungwa kwa shule za umma kwa muda usiojulikana huku zile za watu binafsi zikiendelea na masomo.

Kwa miaka karibu kumi na sita waalimu nchini Kenya wamekuwa wakifanya mgomo wa mara kwa mara kushinikiza madai yao.