UN-DRC-M23

Katibu mkuu wa UN, alitaka jeshi la DRC kuheshimu haki za binadamu pindi linapowakamata waasi wa M23

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa UN, Ban Ki Moon
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa UN, Ban Ki Moon UN Photo/Evan Schneider

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa UN, Ban Ki Moon ameeleza kusikitishwa na namna ambavyo miili ya wapoganaji wa M23 inavyohifadhiwa na namna ambavyo mateka wake wanavyofanyiwa na wanajeshi wa Serikali. 

Matangazo ya kibiashara

Msemaji wa Umoja wa Mataifa UN, Martin Nesirky amesema kuwa katibu mkuu, Ban amehuzunishwa na picha zilizochapishwa na wanajeshi wa Serikali kwenye mtandao kuonesha miili ya waasi wa M23 waliouawa kwenye uwanja wa mapambano.

Kuoneshwa kwa picha hizo kumeyafanya hata mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu nchini humo kuitaka Serikali kutochapisha picha za maiti za wapiganaji wa M23 na badala yake waiifadhi miili yao kwa heshima.

Mbali na kuchapisha picha za miili ya wapiganaji wa M23, jeshi la Serikali pia limechapisha mateka kundi hilo waliojisalimisha kwa vikosi vya Serikali huko mashariki mwa DRC ambako kuna mapigano.

Katibu mkuu Ban ametoa wito kwa Serikali ya DRC kuheshimu haki za binadamu wakati wanajeshi wake wakitekeleza operesheni ya kukabiliana na waasi wa M23 ambao walikuwa wanajaribu kuuteka tena mji wa Goma.

Wachambuzi wa mambo wanaona kuwa kwa sasa kundi la M23 limezidiwa uwezo na wanjeshi hasa baada ya jeshi hilo kupata vifaa vya kisasa na kuwa limejipanga kinyume na ilivyokuwa mwaka uliopita.

Majeshi ya MONUSCO nchini DRC yametaka kuwepo uchunguzi wa kina kubaini iwapo jeshi la Kongo linakiuka haki za binadamu kwa kuwauwa wapiganaji wa M23 pindi likiwakamata, kwakuwa idadi kubwa ya waliouawa huenda waliuawa baada ya kukamatwa.