GUINEA

Serikali ya Guinea yatuma wanajeshi zaidi kusini mwa nchi hiyo kufuatia mapigano ya kikabila

Wanajeshi wa nchi ya Guinea
Wanajeshi wa nchi ya Guinea Reuters

Wanajeshi zaidi wamepelekwa kwenye miji ya kusini mwa nchi ya Guinea kufuatia vifo vya raia 40 vilivyotokana na mapigano ya kikabila. 

Matangazo ya kibiashara

Tayari Serikali ya Guinea imetangaza hali ya hatari kwenye mji wa pili kwa kubwa wa N'Zerekore ambako machafuko haya ndiko yalikoanzia huku wananchi wakipewa wito wa kuwa watulivu.

Vurugu zilizuka baada ya walinzi wa kabila la Guerze kumpiga kijana mmoja wa kabila la Konianke hadi kufa kwa kile walichomtuhumu kuwa alikuwa ni mwizi.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, wamesema kuwa mapigano hayo ya kikabila ni makubwa zaidi kuwahi Kushuhudiwa nchini humo na kwamba kwenye mapigano hayo yaliyodumu kwa siku tatu mfululizo wengi wa waliouawa walinyongwa na wengine kukatwa shingo kwa mapanga.

Licha ya kuongezwa kwa wanajeshi zaidi na polisi, mapigano zaidi yameripotiwa kwenye maeneo ya vijijini ambako wanajeshi bado hawajafanikiwa kufika kutuliza vurugu hizo na mauaji zaidi.

Nchi ya Guinea imekuwa na historia ya kushuhudia mapigano ya kikabila kati ya loo hizi mbili kutokana na Imani za kidini na madai mbali mbali ambayo Serikali yao imeshindwa kuwatimizia.

Wanajeshi zaidi ya laki tatu wanaelezwa kupelekwa kwenye mji wa N'Zerekore ulioko umbali wa kilometa 579 kutoka mji mkuu, Conakry, hali ya hatari imetangazwa kwenye mji huo.

Siku ya Jumanne, rais Alpha Conde kupitia njia ya Televisheni aliwataka wananchi wa maeneo ambako vurugu hizi zilizuka kuwa watulivu wakati huu jeshi likiendelea kurejesha hali ya amani.