KOREA KASKAZINI-PANAMA

Serikali ya Pyongyang yaitaka Panama kuwaachia wafanyakazi wa meli yake

Meli ya Korea Kaskazini  'Chong Chong Gang' ikiwa kwenye bandari ya Panama
Meli ya Korea Kaskazini 'Chong Chong Gang' ikiwa kwenye bandari ya Panama REUTERS/Carlos Jasso

Serikali ya Pyongyang imesisitiza kuwa shehena ya silaha zinazozuiliwa na maofisa usalama wa Panama baada ya kuikamata meli yake kuwa ni mpango halali baina ya nchi hizo mbili. 

Matangazo ya kibiashara

Meli ya Korea Kaskazini ilikamatwa kwenye mfereji ewa bahari ya nchi ya Panama, ambapo mara baada ya kufanyiwa ukaguzi ilibainika kuwa Meli hiyo ilikuwa imesheheni silaha zilizotoka nchini Cuba.

Awali kabla ya kukamatwa kwa Meli hiyo, maofisa wa Serikali ya Cuba walijaribu kuzuia Meli hiyo isikamatwe lakini walichelewa kwakuwa ilikuwa imeshaingia kwenye himaya ya nchi ya Panama.

Ikulu ya Pyongyang hii leo imetoa taarifa kulaani meli yake kushikiliwa pamoja na Sukari ya msaada waliopewa na nchi ya Cuba huku ikitoa wito wa kuachiwa kwa wafanyakazi wa meli hiyo.

Nchi hiyo imeendelea kusisitiza kuwa silaha hizo ni halali na kwamba nyingi ni vifaa ambavyo vingetumika kwenye ukarabati wa silaha nyingine za nchi hiyo ambazo zinahitaji matengenezo.

Serikali ya Panama imeandika barua kwa Umoja wa Mataifa UN ikiutaka itume waangalizi wake kwenda nchini humo kubaini iwapo silaha hizo ni sehemu ya zile ambazo nchi ya Korea Kaskazini imewekewa vikwazo.

Nchi ya Cuba nayo imeiandikia barua Serikali ya Panama kuitaka iwaachie wafanyakazi wa meli ya Chong pamoja na shehena ya sukari ambayo imekamatwa.

Tayari mwendesha mashtaka wa Serikali ya Panama ametangaza kuanza uchunguzi dhidi ya wafanyakazi hao na kwamba iwapo uchunguzi utakamilika watafikishwa mahakamani.