Mawakili wa Alexei Navalny wataka aachiwe huru kupisha kusikilizwa kwa rufaa yao
Imechapishwa: Imehaririwa:
Mawakili wanaomtetea mkosoaji mkubwa wa Serikali ya rais Vladmir Putin, Alexei Navalny wametaka kiongozi huyo kuachiwa huru mpaka pale rufaa yao itakaposikilizwa.
Alexei Navalny aliwekwa kizuizini punde mara baada ya hukumu yake kusomwa ambapo alihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela kwa makosa ya matumizi mabaya ya ofisi.
Mawakili wake wanataka polisi kumuachia Navalny mpaka pale mahakama ya rufaa itakapodhibitisha hukumu yake lakini kwa sasa hapaswi kushikiliwa kwakuwa wamekata rufaa kwenye mahakama kuu.
Hukumu hiyo imelaaniwa vikali na wanaharakati nchini humo wakisema kuwa kesi yake ilichochewa kisiasa kufuatia harakati za kiongozi huyo kuipinga Serikali.
Alexei Navalny alikuwa kinara wa kuitisha maandamano makubwa mjini Moscow kupinga sera za rais Putin na Serikali yake huku akiwatuhumu viongozi wengi kwa kukithiri kwa rushwa.
Wafuasi wake wameandamana kwenye mjii mkuu Moscow wakipinga hukumu hiyo ambayo nao wanadai ni mpango wa Serikali kuwanyamazisha wakosoaji wa Serikali.
Wafadhili wa Alexei Navalny wamesema kufuatia kesi inayomkabili, ametangaza kujiondoa kwenye kinyang'anyiro cha kuwania umeya wa jiji la Moscow kwenye uchaguzi uliopangwa kufanyika mwezi September mwaka huu.
Alexei Navalny amekutwa na hatia ya matumizi mabaya ya ofisi ikiwemo kujipatia fedha kinyume cha sheria wakati akiwa msaidizi wa Gavana katika mji wa Kirov.