MAREKANI-PALESTINA-ISRAEL

Mazungumzo ya amani kati ya Israel na Palestina huenda yasifanyike baada ya mamlaka ya Palestina kutoa masharti kabla ya kuzungumza na Israel

Mtoto raia wa Palestina akijaribu kuwasukuma wanajeshi wa Israel kwenye eneo la ukanda wa Gaza
Mtoto raia wa Palestina akijaribu kuwasukuma wanajeshi wa Israel kwenye eneo la ukanda wa Gaza REUTERS/Ammar Awad

Mazungumzo ya amani kati ya mamlaka ya Palestina na Serikali ya Israel yameingia dosari baada ya viongozi wa Palestina kutaka kwanza wakubaliane kushirikiana kwenye maeneo ya mpaka. 

Matangazo ya kibiashara

Ujumbe wa Palestina umesema kuwa kabla ya wao kushiriki mazungumzo ya amani na Israel ni lazima weakubaliane na Israel katika ushirikiano wa mipaka na hali ijayo ya taifa la Palestina.

Palestina ilimtuma mduluhishi wake, Saeb Erekat kukutana na waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, John Kerry kumueleza msimamo wa Palestina kuhusu mzozo wa mpaka kabla ya kuingia kwenye meza ya mazungumzo.

Hata hivyo Serikali ya Israel na yenyewe imesema haiko tayari kushiriki kwenye mazungumzo ambayo Palestina inatoa masharti kabla ya kushiriki mazungumzo.

Mamlaka ya Palestina inataka eneo la ukanda Gaza na Jerusalemu mashariki yawe kwenye himaya yao kulingana na mkataba wa mwaka 1967 ambao ulianisha maeneo hayo kuwa ardhi ya Palestina.

Palestina inataka kuhakikishiwa umiliki wa maeneo hayo ambayo iwapo utaridhiwa utaifanya Serikali ya Israel kusitisha ujenzi wake wa makazi ya kudumu kwenye eneo la ukanda wa Gaza.

Waziri Kerry anatarajiwa kukutana na pande hizo mbili kwa mara nyingine hii leo kabla hajasafiri kurejea nyumbani.

Serikali ya Marekani imesema itasimama kidete kuhakikisha pande hizo mbili zinaridhiana kuhusu maeneo ya mpaka ili kumaliza machafuko ambayo yamekuwa yakishuhudiwa kati ya nchi hizo mbili.