MISRI-EU

Muslim Brotherhood waonesha nia ya kushiriki mazungumzo na Serikali licha ya kuitisha maandamano zaidi

Wafuasi wanaomuunga mkono Mohamed Morsi wakiandamana mjini Cairo
Wafuasi wanaomuunga mkono Mohamed Morsi wakiandamana mjini Cairo REUTERS

Chama cha Muslim Brotbherhood cha nchini Misri, kimetangaza kufanya maandamano zaidi kupinga mapinduzi ya kijeshi yaliyofanyika nchini humo.Usiku wa kuamkia leo, maelfu ya wafuasi wa chama hicho waliendelea kuonekana kwenye miji mbalimbali ikiwemo mjini Cairo na Alexandria huku wakiapa mkusanyiko mkubwa zaidi mara baada ya sala ya Ijumaa. 

Matangazo ya kibiashara

Maandamano haya yanaitishwa huku jeshi nchini Misri likionya dhidi ya maandamano ya vurugu na kwamba halitasita kuchukua hatua dhidi ya waandamanaji wakorofi wanaotumia maandamano hayo kufanya fujo.

Kwa upande wake rais wa mpito Adly Mansour, amesema hatoangalia nchi yake ikiteketea kwa vurugu za watu wachache na kwamba atahakikisha anailinda Misri kwa namna yoyote.

Msemaji wa chama cha Muslim Brotherhood, Gehad el-Haddid amesema kuwa chama chake hakikotayari kwa mazungumzo na Serikali mpaka pale jeshi litakapomrejesha madarakani Mohamed Morsi.

Hata hivyo wakati chama hicho kikiweka ngumu kushiriki mazungumzo ya kutafuta suluhu na Serikali ya mpito, baadhi ya vyama vya upinzani vilivyokuwa vinapinga mapinduzi hayo vimeonesha nia ya kutaka kushiriki mazungumzo.

Ujumbe wa Umoja wa Ulaya ulikuwepo nchini Misri juma hili umesema baada ya kukutana na wawakilishi wa Morsi, chama hicho kimependekeza njia za kufanywa ili kumaliza machafuko nchini Misri.

Kiongozi wa ujumbe wa Umoja wa Ulaya EU, Bernardino Leon amesema licha ya kukutana na pande hizo mbili, bado viongozi wao wanatofautiana sana katika kutafuta suluhu ya Misri.