DRC

Raia wa 4 wa DRC wapandishwa kizimbani mjini Kinshasa kwa kujifanya wakuu wa nchi

Rais wa DRC, Josephu Kabila
Rais wa DRC, Josephu Kabila Reuters

Watu wanne wanaodaiwa kuwa ni matapeli waliokuwa wakijifanya ni rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC, wamekamatwa na polisi mjini Kinshasa na kupandishwa kizimbani hii leo. 

Matangazo ya kibiashara

Taarifa iliyotolewa na wizara ya mambo ya ndani ya DRC, inasema kuwa mmoja wa watuhumiwa hao alikuwa akijifanya kama rais Joseph Kabila na kuwadanganya baadhi ya wafanyabishara kuwa angewawezesha kufanya kirahisi biashara ya madini.

Kukamatwa kwa watuhumiwa hao kunakuja baada ya mmoja wa waathirika wa mtandao huo wa kitapeli kudai kuwa alipigiwa simu na rais Joseph Kabila akimtaka alipe dola milioni 3 ili aweze kumpatia kibali cha kuchimba madini jambo ambalo mfanyabiashara huyo alitekeleza.

Mbali na watu hao kuwatapeli wafanyabiashara inadaiwa kuwa pia walijifanya ni maofisa wa juu wa jeshi la Kinshasa ambapo mara kadhaa waliandika barua kwa vikosi vya mjini Goma kurudi nyuma kutoa nafasi kwa waasi wa M23 kuingia kirahisi mjini Goma.

Wafanyabiashara hao walilalamika kwa Ikulu ya Kinshasa wakitaka kuonana na rais Josephu Kabila kumueleza masikitiko yao kutokana na rais kutotekeleza ahadi yake jambo ambalo ikulu ya Kinshasa imekanusha kuandika barua za aina hiyo.

Watuhumiwa hao walisharipotiwa toka mwaka 2012 lakini walikuwa hawajakamatwa kutokana na kulindwa na baadhi ya viongozi hadi pale polisi walipoagizwa kuwakamata na kuwafikisha mahakamani kujibu mashtaka yanayowakabili.