CHINA

Watu 73 wapoteza maisha nchini China baada ya Jimbo la Gansu kupigwa na matetemeko mawili ya ardhi

Wananchi wa Jimbo la Gansu nchini China wakiwa wamekimbia makazi yao baada ya eneo hilo kupigwa na tetemeko la ardhi
Wananchi wa Jimbo la Gansu nchini China wakiwa wamekimbia makazi yao baada ya eneo hilo kupigwa na tetemeko la ardhi

Watu sabini na watatu wamepoteza maisha nchini China baada ya Taifa hilo kupigwa na matetemeko mawili ya ardhi yaliyochangia kuwaacha watu wengine zaidi ya mia nne wakijeruhiwa.

Matangazo ya kibiashara

Matetemeko hayo ya ardhi yamechangia majengo 21,000 kupata madhara huku mengine zaidi ya 1,200 yakiharibiwa kabisa katika Jimbo la Gansu linalopatikana kwenye Jiji la Dingxi.

Mamlaka nchini China zimekiri kumekuwa na uharibifu mkubwa uliochangiwa na matetemeko hayo mawili yaliyokuwa na ukubwa wa vipimo vya matetemeko vya 5.9 na 5.6.

Kikosi cha Ukoaji kimeendelea na kazi ya kufukua mabaki ya vifusi vilivyochangiwa na kubomoka kwa nyumba hizo wakiangaliaiwapo kuna maiti zozote au manusura ambao wamebanwa.

Zaidi ya wanajeshi 2,000, askari 300, Madaktari 50 na Helkopta mbili zimejumuishwa kwenye zoezi hilo la uokozi likiwa na lengo na kusaka watu ambao bado wapo hai sanjari na kufukua vifusi hivyo.

Makamu Meya wa Jiji la Dingxi amekiri zoezi la ukoaji zinakwenda vizuri kutokana na uwepo wa vifaa vote muhimu ambavyo vinahitajika kwa ajili ya kukabiliana na hali yoyote ambayo inaweza ikawa kikwazo.

Taarifa zinaeleza kuna baadhi ya nyumba ambazo zimeharibiwa kabisa baada ya kufukiwa kutokana na kuwa karibu na majengo marefu yaliyokuwa bado yanajengwa na hivyo matofali kuangukia nyumba hizo.

China ni miongoni mwa mataifa ambayo yamekuwa yakikabiliwa na matetemeko ya ardhi ya mara kwa mara kitu ambacho kimekuwa kikichangia vifo vya watu na uharibifu wa mali za raia.