VENEZUELA

Mahakama ya juu nchini Venezuela yatupilia mbali rufaa ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa mwezi April

Henrique Capriles kiongozi mkuu wa upinzani nchini Venezuela
Henrique Capriles kiongozi mkuu wa upinzani nchini Venezuela ©Reuters.

Mahakama ya juu nchini Venezuela imetupilia mbali rufaa iliyokatwa na kiongozi wa upinzani nchini humo, Henrique Capriles akipinga matokeo ya urais kwenye uchaguzi wa mwezi April mwaka huu.

Matangazo ya kibiashara

Majaji waliokuwa wanasikiliza kesi hiyo wamesema kuwa kesi iliyowasilishwa na kiongozi wa upinzani haina mashiko na kwamba hakuna uwezekano wa kusikilizwa kutokana na kuwa na mapungufu mengi.

Mara baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Capriles aliandika kwenye mtandao wake wa kijamii wa Twitter "Lack of Justice" akimaanisha nchini mwake kuna mapungufu ya haki ya kisheria.

Capriles aliwasilisha kesi yake mahakamani punde baada ya matokeo kutangazwa akipinga ushindi wa Nicolas Maduro aliyeshinda kwenye uchaguzi uliokuwa wakuziba pengo la rais Hugo Chavez aliyefariki kwa maradhi ya saratani.

Mwezi June mwaka huu tume ya taifa ya uchaguzi mara baada ya kufanya uchunguzi wake ilibaini kuwa Maduro alishinda kwa kura milioni, uchunguzi ambao hata hivyo upinzani unapinga na kudai ulikuwa bandia.

Rais Maduro alishinda kwenye kinyang'anyiro hicho kwa asilimia 1.5 ambayo ni tofauti ya kura laki mbili na mpinzani wake Henrique Capriles.

Kwenye hukumu yake jaji, Gladys Gutierrez amesema upande wa mashtaka ulishindwa kuwasilisha ushahidi wa kutosha kuweza kusikiliza kesi ya kupinga matokeo huku akisema vidhibiti vilivyowasilishwa na upinzani vilikuwa na mapungufu mengi.

Capriles amesema amekosoa hukumu ya mahakama akisisitiza kuwa hukumu yake haikuwa na usawa kwakuwa ilicheleweshwa kutolewa na kwamba atawasilisha malalamiko yake kwenye mahakama za kimataifa ili apate haki.