CAIRO-MISRI

Marekani na Umoja wa Ulaya waonya kuhusu kuendelea kushuhudiwa kwa mzozo wa kisiasa nchini Misri

Waandamanaji mjini Cairo Misri wanaomuunga mkono Mohamed Morsi
Waandamanaji mjini Cairo Misri wanaomuunga mkono Mohamed Morsi REUTERS/Mohamed Abd El Ghany

Serikali ya Marekani na Jumuiya ya Umoja wa Ulaya EU umeonya kuhusu kuendelea kuzorota kwa hali ya kisiasa nchini Misri saa chache baada ya Serikali ya mpito kutangaza kuwa suluhu ya kimataifa imeshindikana.

Matangazo ya kibiashara

Kwenye taariofa yao ya pamoja, Marekani na Umoja wa Ulaya zimeitaka serikali ya mpito kuhakikisha inamaliza tofauti ya kisiasa iliyoko nchini humo kwakuwa wao kwa sehemu kubwa wanapaswa kulaumiwa kwa kile kinachoendelea kushuhudiwa.

Kauli ya Marekani na Umoja wa Ulaya inakuja saa chache baada ya kuendelea kushuhudiwa maandamano makubwa ya wafuasi wanaomuunga mkono Mohamed Morsi aliyeondolewa madarakani na jeshi.

Serikali ya Misri imetangaza kuwa itawasambaratisha waandamanaji wote watakaoendelea kusalia kwenye maeneo ambayo awali walitakiwa kuondoka kwakuwa kuendelea kusalia kwenye maeneo hayo kunafanya hali kuwa mbaya zaidi nchini humo.

Waandamani wanaomuunga mkono rais Mohamed Morsi wamesisitiza kutotii amri ya jeshi la ile iliyotangazwa na Serikali ya kuwataka waondoke kwenye maeneo ambayo wanayakalia mpaka hivi sasa.

Mamia ya raia wameuawa mpaja sasa toka kupinduliwa madarakani kwa Mohamed Morsi tarehe 3 ya mwezi July mwaka huu ambapo jeshi linashika hatamu.

Toka wakati huo, wasuluhishi wa Marekani, Umoja wa Ulaya EU, Qatar na nchi za falme za kiarabu zimefanya juhudi kujaribu kuzishawishi pande mbili zinazokinzana nchini humo kurejea kwenye meza ya mazungumzo.

Hata hivyo inaonekana juhudi za mataifa hayo zimegonga mwamba kutokana na kuendelea kushuhudiwa kwa maandamano ya upande wanaoiunga mkono Serikali ya mpito na wale wanaomuunga mkono rais Mohamed Morsi.

Ofisi ya rais wa mpito, Adly Mansour imetoa taarifa ikieleza kushindikana kwa juhudi za kimataifa kujaribu kumaliza mzozo huo huku wakiwabebesha lawama wafuasi wa chama cha Muslim Brotherhood kwa kuchangia mazungumzo hayo ya kusaka suluhu kushinidikana.