KENYA-NAIROBI

Safari za ndege za kimataifa zaanza tena kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta nchini Kenya

Sehemu ya uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta mjini Nairobi iliyoungua hapo jana
Sehemu ya uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta mjini Nairobi iliyoungua hapo jana Reuters

Safari za ndege za Kimataifa hatimaye zimeanza tena katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta nchini Kenya kufuatia hapo jana kusitishwa kutokana na ajali ya moto kwenye uwanja huo.

Matangazo ya kibiashara

Hapo jana Serikali ya Kenya ilitangaza kusitisha safari zote za kimataifa kwenye uwanja huo kutokana na kuungua kwa sehemu ya uwanja hasa kwenye eneo la kuwasili kwa abiria wa kimataifa pamoja na idara ya uhamiaji.

Ndege nyingi hapo jana zilizokuwa zikitarajiwa kutumia uwanja huo zililazimika kukatisha safari zao na kuelekea kwenye nchi jirani za Tanzania na Uganda huku baadhi zikielekezwa kwenye uwanja wa kimataifa wa Moi mjini Mombasa.

Rais Uhuru Kenyatta pamoja na waziri wa masuala ya usafiri wa Kenya hapo jana waliahidi kufanya kila linalowezekana ili kufanikisha kurejeshwa kwa safari za kimataifa kwenye uwanja huo jambo ambalo limeanza kushuhudiwa hii leo.

Ndege ya kwanza kutua ilikuwa ikitokea nchini Uingereza na kutua majira ya ya saa kumi na mbili na nusu kwa saa za Afrika Mashariki.

Ndege nyingine zilizoshuhudiwa zikitua kwenye uwanja huo ni pamoja na zile zilizotoka nchini Bangkok na kilimanjaro nchini Tanzania hali ambayo sasa inatoa matumaini ya kurejea kwa safari nyingi hii leo.

Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta ni uwanja mkubwa zaidi kutumika kwenye kanda hii ya Afrika Mashariki ambapo huudumia zaidi ya abiria elfu kumi na sita kwa siku.

Wataalamu wa masuala ya uchumi wanasema kuwa kutokana na kuungua kwa sehemu ya uwanja huo na kusitishwa kwa safari nyingi hapo jana kumeathiri kwa kiasi hali ya uchumi wa taifa hilo kwakuwa uwanja huo umetegemewa kwa kuingiza watalii wengi zaidi.

Shughuli za usafiri wa Tax zilikosa wateja kutokana na moto huo huku wachuuzi wa barabarani pia nao wakidai kuathirika kutokana na ajali hiyo.

Safari za ndege za ndani zenyewe zilianza hiyo jana mara baada ya moto mkubwa kudhibitiwa.

Moto huo ulianza majira ya saa kumi za alfajiri usiku wa Jumatano na kusababisha kuunguza sehemu kubwa ya idara ya uhamiaji na sehemu ya kuingilia abiria wa kimataifa.

Uchunguzi tayari umeanza kubaini chanzo cha moto huo.