MOSCOW-URUSI

Urusi yasikitishwa na hatua ya rais Obama kusitisha ziara yake mjini Moscow mwezi ujao

Rais wa Urusi,Vladmir Putin
Rais wa Urusi,Vladmir Putin REUTERS/Maxim Shemetov

Rais wa Urusi Vladmir Putin ameeleza kusikitishwa na hatua ya rais wa Marekani Barack Obama kutangaza kusitisha ziara yake nchini humo kuhudhuria mkutano kati yake na rais Putin.

Matangazo ya kibiashara

Rais Putin amesema kuwa ameshangazwa na hatua ya Obama kutangaza kusitisha mkutano wake nchini Urusi kwasababu ya mtu mmoja ambae wanamtuhumu kuvujisha siri za taifa hilo.

Rais Obama amesema kuwa hawezi kwenda nchini Urusi kwakuwa nchi hiyo imeendelea kumuhifadhi Edward Snowden jasusi wa zamani wa Marekani aliyevujisha siri za taifa hilo.

Mshauri wa rais Putin, Yuri Ushakov amewaambia waandishi wa habari mjini Moscow kuwa hatua ya Marekani inadhihirisha ni jinsi gani taifa hilo linavyoshindwa kuendeleza uhusiano wa kimataifa na nchi yao kwa kuingiza masuala binafsi.

Mshauri huyo ameongeza kuwa mwaliko wa rais Putin kwa rais Obama mwezi ujao utaendelea kusalia palepale na kwamba wao wako tayari kuendeleza uhusiano ulipo kati ya mataifa hayo mawili.

Marekani na Urusi zimeingia kwenye mzozo wa maneno kufuatia hivi karibuni taifa hilo kukubali kumpatia hifadhi ya mwaka mmoja nchini humo, Edward Snowden ambaye awali alikuwa amekwama kwenye uwanja wa ndege mjini Moscow kutokana na kukosa nyaraka ambazo baadae alikabidhiwa na Serikali ya Urusi.

Kwenye mkutano wake na waandishi wa habari, rais Obama amesema kuwa anashangazwa na nchi ya Urusi kuwa na mtindo wa kuendeleza vita baridi ambayo imepitwa na wakati na kusisitiza kuwa ataenda nchini humo iwapo watakubaliana kuhusu Edward Snowden.

Urusi imesisitiza kuwa iliamua kumpatia hifadhi Snowden kwasababu za kibinaadamu na ilifanya hivyo vila kuangalia ushirikiano wa mataifa hayo mawili kwakuwa waliamini suala la Snowden haliwezi kuathiri ushirikiano wao.