ISRAEL-PALESTINA-IRAN-MAREKANI

Ayatollah Ali Khamenei akashifu kuanza tena kwa mazungumzo ya amani kati ya Israel na Palestina

Kiongozi wa juu wa kidini wa Iran, Ayatolla Ali Khamenei
Kiongozi wa juu wa kidini wa Iran, Ayatolla Ali Khamenei REUTERS/Hamid Forootan/ISNA

Kiongozi wa juu wa kidini nchini Iran, Ayatollah Ali Khamenei hii leo ameionya nchi ya Palestina dhidi ya kuanzisha tena mazungumzo ya amani kati yake na Israel, akisema kufanya hivyo kutifanya ipoteze haki zake.  

Matangazo ya kibiashara

Khamenei amesema kuwa iwapo Palestina itakubali kuanza mazungumzo mapya na Serikali ya Israel basi ni wazi mwisho wa siku wao ndio watakaoumia na sio taifa la Israel wala Marekani ambao wanamalengo sawa kuhusu eneo la ukanda wa gaza.

Akizungumza kwenye msikiti wa chuo kikuu cha Tehran wakati wa sala ya Eid al-Fitr, Ali Khamenei amesema kuwa kujiingiza kwenye mazungumzo hayo kwa viongozi wa Palestina kutasababisha wakose haki zao za msingi na kuwanufaisha Israel ambao wanataka kuona taifa lao likiteketea.

Kauli ya Ali Khamenei inakuja ikiwa imepita siku moja toka ofisi ya wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani, itangaze kuwa wapatanishi wa mgogoro kati ya Israel na Palestina watakutana tarehe 14 ya mwezi huu kwa mazungumzo mengine mjini Jerusalem.

Mazungumzo kati ya pande hizi mbili yalianza mwezi mmoja uliopita lakini yakavunjika katika dakika za mwishi baada ya wapatanishi wa Israel na Palestina kutokukubaliana kwenye baadhi ya mambo.

Hivi karibuni waziri wa mambo ya Kigeni wa Marekani John Kerry alinukuliwa akileza matumaini yake kwenye mazungumzo ya safari hii akiamini kuwa huenda yakafua dafu ili kumaliza mzozo kati ya mataifa hayo mawili kuhusu eneo la ukanda wa gaza.

Nchi ya Iran imekuwa mstari wa mbele katika kutoa msaada mkubwa kwa kundi la kiislamu la Hamas nchini Palestina ambalo linapinga sera za Israel kuhusu eneo la ukanda wa Gaza.