UMOJA WA ULAYA-MISRI

Umoja wa Ulaya EU waiwekea vikwazo vya silaha serikali ya Misri kufuatia umwagaji wa damu unaendelea kushuhudiwa nchini humo

William Hague,waziri wa mambo ya nje wa Uingereza na Catherine Ashton, mkuu wa sera za mambo ya nje wa EU wakati wa kikao cha jijini Brusels juu ya Misri Agosti 21, 2013.
William Hague,waziri wa mambo ya nje wa Uingereza na Catherine Ashton, mkuu wa sera za mambo ya nje wa EU wakati wa kikao cha jijini Brusels juu ya Misri Agosti 21, 2013. REUTERS/Francois Lenoir

Umoja wa Ulaya EU hapo jana umetangaza kuweka vikwazo vya kuiuzia silaha na vifaa vya kijeshi nchi ya Misri kufuatia machafuko yaliyoshuhudiwa juma moja lililopita lakini ukasisitiza kuendelea na msaada wake wa kiuchumi kwa taifa hilo.

Matangazo ya kibiashara

Mawaziri wa mambo ya kigeni wa Umoja wa Ulaya wamelaani vikali machafuko yanayoendelea na ambapo mpaka sasa watu zaidi ya elfu moja wanadaiwa kuuawa toka kuanza kwa operesheni ya kuwaondoa waandamanaji mjini Cairo juma lililopita

Mkuu wa sera za mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton amesema kwamba anataka apewe nafasi nyingine kusuluhisha mzozo wa Misri na kutoa wito wa amani.

Katika hatuwa nyingine, Mahakama moja nchini Misri imeagiza kuachiwa huru kwa rais wa zamani wa taifa hilo Hosni Mubarak ambaye amefutiwa makosa ya rushwa na sasa atakuwa kwenye kifungo cha nyumbani akisubiri kesi ya kuamrisha mauaji dhidi ya waandamanji inayonkabili.

Saa chache baada ya uamuzi wa mahakama, waziri mkuu Hazem al-Beblawi ambaye pia ni kaimu mkuu wa majeshi, aliagiza kiongozi huyo kuwa chini ya ulinzi akiwa nyumbani kwake akisubiri kesi nyingine za rushwa zinazomkabili.

Wachambuzi wa mambo wanaona kuwa kuna dalili zote za kiongozi huyo kuachiwa huru licha ya kesi ya mauaji ya waandamanji zaidi ya 850 waliouawa wakati wa maandamano ya kuuangusha utawala wake mwaka 2011.