SYRIA-MAREKANI

Syria yasema Marekani inaidanganya dunia kuhusu silaha za kemikali

Waziri wa Mambo ya nje wa Syria Walid Moualem ameitaka dunia kutoa ushahidi kuwa serikali yake ilitumia silaha za kemikali wiki iliyopita dhidi ya wapinzani na kusababisha vifo vya mamia ya watu mjini Damascus.

Matangazo ya kibiashara

Moualem ameongeza kuwa serikali ya Marekani na washirika wake wanaidanganya dunia kuwa wamethibitisha kuwa silaha hizo zilitumiwa dhidi ya waasi kwa sababu wanatafuta njia ya kuingia nchini humo, na kuongeza kuwa wako tayari kujilinda ikiwa watashambuliwa.

Nchi za Urusi na Iran nazo zimesema kuwa hatua yeyote ya kijeshi dhidi ya Syria bila ya kupitia katika baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa haikubaliki na ni kinyume cha sheria za kimataifa.

Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameroon ameitisha kikao cha dharura cha wabunge siku ya Alhamisi kujadili mustakabali wa Syria kipindi hiki dalili zikionesha kuwa mataifa ya Magharibi yakiongozwa na Marekani yanajiandaa kuivamia Syria.

Duru kutoka Washington DC zinasema kuwa jeshi la Marekani lipo tayari kuongoza mashambulizi hayo, huku uongozi wa upinzani nchini Syria ukisema kuwa umeambiwa kuwa watarajie mashambulizi  dhidi ya serikali ya rais Assad katika siku kadhaa zijazo.

Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani John Kerry amesema kuwa kilichotokea nchini Syria hakikubaliki kamwe na ni lazima serikali ya rais Bashar Al Assad iwajibike kwa mauaji hayo.

Marekani na washirika wake kama Ufaransa na Uingereza wanasema wakati umefika kwa Syria kuvamiwa kijeshi pendekezo ambalo washirika wa karibu wa rais Assad China na Urusi wanapinga.

Leo ni siku ya pili ya uchunguzi unaofanywa na watalaam wa Umoja wa Mataifa kubaini ikiwa kweli silaha za kemikali zilitumiwa dhidi ya raia wasiokuwa na wakati.

Rais Bashar Al Assad amesema kuwa tishio la Marekani kuwa ikiwa uchunguzi utabaini kuwa silaha hizo zilitumiwa, italazimika kuingilia mzozo huo kijeshi ni jambo ambalo halikubaliki kamwe.

Akihojiwa na gazeti la kila siku la Urusi la Izvestia Assad amesisitiza kuwa Marekani haitafaulu na kamwe hawezi kuwa kibaraka cha mataifa ya Magharibi na ataendelea kupambana na makundi ya kigaidi yanayolenga kuiangusha nchi yake.

Mwaka uliopita, rais Obama alionya kuwa ikiwa serikali ya Syria itatumia silaha za kemikali dhidi ya wapinzani , nchi yake itaivamia kijeshi.

Waziri wa Mambo ya nje wa Uingereza William Hague naye amesema kuwa ikiwa silaha hizo zilitumiwa ni sharti hatua zichukuliwe lakini anahofia kuwa huenda ushahidi wa kufahamu ukweli umeshaharibiwa.

Serikali ya Assad imeendelea kusisitiza kuwa haiwezi na haijawahi kutumia silaha za kemikali dhidi ya wapinzani na itafanya hivyo ikiwa nchi yake itavamiwa na watu kutoka nje.

Machafuko nchini Syria yamesabisha zaidi ya watu Laki Moja kupoteza maisha kwa kipindi cha miaka miwli iliyopita kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, na Mamilioni kusalia kuwa wakimbizi wakiwemo watoto.

Suluhu ya mzozo wa Syria inasalia kuwa kitendawili baada ya juhudi za Kidiplomasia kugonga mwamba.