UFILIPINO

Jeshi nchini Ufilipino lauzingira mji unaoshikiliwa na waasi wa MNLF

Wanajeshi wa Ufilipino wameuzingira mji wa Zamboanga ulioko kusini mwa nchi hiyo tayari kukabiliana na wapiganaji wa kiislamu wenye silaha ambao mwishoni mwa juma waliwaua watu zaidi ya sita na kuwashikilia mateka wengine 20.

Rais wa Ufilipino, Benigno Aquino
Rais wa Ufilipino, Benigno Aquino Reuters
Matangazo ya kibiashara

Wachambuzi wa mambo wanaseam kuwa tukio lililofanywa na wapiganaji hao wakiislamu linalenga kukwamisha mazungumzo ya amani yanayoendelea kati ya Serikali ya Ufilipino na waasi wa jimbo hilo.

Msemaji wa jeshi la Ufilipino, Luteni Kanali, Ramon Zagala amedhibitisha kuvamiwa vijiji kadhaa vya mji huo na wapiganaji wa kiislamu wenye silaha wapatao 300 ambao wanaunda kundi la Moro Natioanl Liberation Front.

Msemaji huyo amesema kuwa wapiganaji hao wanajaribu kuingia katikati ya mji wa Zamboanga na kwamba jeshi la nchi hiyo halitakubali kuona waasi hao wakifanikisha malengo yao.

Tayari rais Benigno Aquino ametoa taarifa kulaani mashambulizi yaliyofanywa na wapiganaji hao, akisema yanalenga kukwamisha mazungumzo yatakayomaliza vita vilivyodumu kwa zaidi ya miaka 42 nchini humo na ambapo watu elfu 15 wamepoteza maisha mpaka sasa.

Msemaji wa rais Aquino, Edwin Lacierda amesema kuwa tayari rais ametoa amri kwa wanajeshi kuwadhibiti wapiganaji hao kuingia kwenye maeneo ya mijini na kuliagiza jeshi kuhakikisha raia hawaathiriwi na mapigano yanayoendelea.

Milio ya risasi na mabomu imesikika kwenye miji jirani na mji ambao waasi hao wanaushikilia hali ambayo inazusha hofu kwa wananchi wake wapatao milioni moja wanaoishi kwenye eneo hilo.

Maduka na baadhi ya shule zilitangazwa kufungwa kwenye mji wa Zamboanga ambao mara kwa mara umeshuhudia kundi la waasi wa Kiislamu wakiuvamia na kuuteka kwa miongo kadhaa.