DRC-M23-FDLR-RWANDA

M23: Tuko tayari kusalimisha silaha iwapo madai yetu yatatekelezwa na Serikali ya Kinshasa

Kiongozi wa kisiasa wa kundi la waasi wa M23 nchini DRC, Betrand Bisimwa
Kiongozi wa kisiasa wa kundi la waasi wa M23 nchini DRC, Betrand Bisimwa Reuters

Kiongozi wa kisiasa wa kundi la waasi wa M23 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC, Betrand Bisimwa amesema kundi lake liko tayari kusalimisha silaha kwa masharti kwamba wakimbizi wa Kongo warejee nyumbani pamoja na kuondolewa kwa wapiganaji wa kihutu wa FDLR.

Matangazo ya kibiashara

Kiongozi huyo wa kundi la M23 ambalo limekuwa kwenye mapambano na wanajeshi wa Serikali wa FRDC kwa zaidi ya mwaka mmoja, amesema watakuwa tayari kurejea kwenye maisha ya kawaida iwapo madai yao yatatekelezwa na Serikali ya Kinshasa kwenye mazungumzo yanayotarajiwa kuanza mjini Kampala Uganda.

Betrand Bisimwa amesema kuwa wapiganaji wao watakuwa tayari kusalimisha silaha iwapo swala wa waasi wa kihutu wa FDLR litashughulikiwa na kumalizwa pamoja na wakimbizi wa Kongo walioko kwenye makambi ya Rwanda, Uganda na Burundi watarejea nyumbani.

Madai ya M23 yanatolewa wakati huu ambapo viongozi wa nchi za maziwa makui wamemaliza mkutano wao mjini Kampala juma lililopita ambapo waliziagiza pande hizo mbili kusitisha mapigano na kutejea kwenye meza ya mazungumzo.

Waasi wa M23 na Serikali ya Kinshasa walitiliana saini ya kusitisha mapigano mwaka 2009 lakini makubaliano hayo yalivunjika baada ya waasi hao kudai kuwa madai yaliyotiwa saini na Serikali hayakutekelezwa.

Umoja wa Mataifa na makundi mengine ya kutetea haki za binadamu nchini DRC wanalituhumu kundi la waasi wa M23 kwa kuendesha mapigano mashariki mwa nchi hiyo pamoja na kutekeleza vitendo vingi vya ukiukaji wa haki za binadamu.

Umoja wa Mataifa pia unaituhumu nchi ya Rwanda kwakuwa mstari wa mbele kuwafadhili waasi hao kwa silaha ambazo wamekuwa wakiziingiza mashariki mwa nchi hiyo kimagendo na kuwafikia waasi hao.

Serikali ya Rwanda yenyewe mara kadhaa imekanusha kuhusika na ufadhili wa silaha kwa waasi wa M23.

Baadhi ya wapiganaji na viongozi wa kundi la FDLR wanasakwa na mahakama ya kimataifa ya Uhalifu wa kivita ICC wakituhumiwa kuhusika na mauaji ya wahutu na watutsia nchini Rwanda na Burundi, machafuko yaliyoshuhudiwa watu laki 8 wakipoteza maisha.