SYRIA-MAREKANI-URUSI

Rais Assad aionya Marekani dhidi ya mashambulizi ambayo inapanga kuyafanya nchini mwake

Rais wa Syria, Bashar al-Assad ameionya nchi ya Marekani dhidi ya kuishambulia nchi yake kufuatia tuhuma kuwa Serikali yake imetumia silaha za kemikali dhidi ya raia wake, wakati huu ambapo rais Obama anaendelea kusaka uungwaji mkono kuchukua hatua za kijeshi.

Rais wa Syria, Bashar al-Assad
Rais wa Syria, Bashar al-Assad Reuters
Matangazo ya kibiashara

Kwenye mahojiano maalumu na kituo cha televisheni cha Marekani, CBS, rais Assad amesema kuwa kuishambulia kijeshi nchi yake kunamaanisha uchokozi dhidi ya nchi marafiki wa Syria ambao wanaunga mkono Serikali yake.

Rais Assad pia amekanusha Serikali yake kuhusika na shambulio la kemikali lililotekelezwa majuma kadhaa yaliyopita akisema kuwa jeshi lake halijafanya shambulio hilo na kuwa hakuna ushahidi wa kutosha kudhibitisha madai ya Marekani.

Kiongozi huyo amesisitiza kuwa Marekani haina ushahidi wowote kudhibitisha madai yao kuwa wanajeshi wake walitumia silaha za kemikali na kwamba huo ni mpango wa rais barack Obama kutaka kuivamia kijeshi nchi yake.

Kati ahatua nyingine wizara ya mambo ya kigeni ya Urusi imetoa taarifa kuonesha kuwa rais Assad ameishukuru Serikali ya Urusi kwa kuendelea kuinga mkono Serikali yake na kupinga mashambulizi yoyote yanayotaka kufanywa dhidi ya nchi yake.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry amekanusha madai ya rais Assad kuwa nchi yake haina ushahidi wa kutosha dhidi ya Syria na kusisitiza kuwa Marekani itaendelea na ushawishi wake kuhusu uvamizi wa kijeshi dhidi ya Syria.