AUSTRALI

Waziri mkuu mteule wa Australia, Tony Abbott aanza kazi, akabiliwa na changamoto kwenye bunge la Seneti

Waziri mkuu mteule wa Australia, Tony Abbott
Waziri mkuu mteule wa Australia, Tony Abbott Reuters

Waziri mkuu mteule wa Australia, Tonny Abbott hii leo ameanza kazi huku akikabiliwa na changamoto nyingi za sheria ambazo zilipitishwa na chama kilichoondolewa madarakani cha Labour.

Matangazo ya kibiashara

Tayari waziri mkuu Abbott ameanza kazi ya kutengeneza baraza lake la mawaziri ambalo linaunda serikali mpya baada ya uchaguzi wa kihistoria ulioshuhudia kumalizika kwa utawala wa miaka sita wa chama cha Labor.

Licha ya ushindi alioupata mwishoni mwa juma, waziri mkuu Abbott anakabiliwa na changamoto za upitishwaji wa sheria na mabadiliko ya serikali yake ambayo yatalazimika kupitishwa kwenye bunge la Seneti ambalo kwa sehemu kubwa linawabunge wengi wa Labor.

Abbott ambaye alikuwa mpinzani wa waziri mkuu anaeondoka madarani Kevin Rudd anaelezwa na wachambuzi wa mambo kuwa mmoja kati ya viongozi wenye mvuto kwa wananchi ingawa atakabiliwa na changamoto nyingi kwenye vyombo vya kutunga sheria.

Akizungumza na wanahabari kwa mara ya kwanza mjini Canibera, waziri mkuu Abbott ameahidi kufanya mabadiliko makubwa kwenye serikali yake ikiwemo kubadili baadhi ya sheria ambazo zinaonekana kuyabana makampuni na wananchi.

Wakati wa kampeni ajenda kubwa ya waziri mkuu Abbott ilikuwa  ni namna ya kukabiliana na wimbi la wakimbizi wanaoingia nchini humo kwa kutumia boti wakitokea nchini Indonesia ambapo hii leo boti iliyokuwa na wakimbizi zaidi ya 140 ilikamatwa na maofisa usalama wa Australia.

Hata hivyo wachambuzi wa mambo wanaona kuwa waziri mkuu Abbott atapata uungwaji mkubwa kwenye bunge ambalo linawabunge wengi wa muungano wa Loberal ambao wanaviti 32 huku kwenye bunge la Seneti hali ikiwa bado haijajulikana kwenye mgawanyo wa viti.