SYRIA-MAREKANI-URUSI-IRAN

Iran na Marekani zakubaliana na mpango wa Urusi kutaka Syria kuteketeza silaha zake za kemikali

Rais wa Marekani, Barack Obama
Rais wa Marekani, Barack Obama Reuters

Nchi ya Iran imekaribisha kwa mikono miwili mapendekezo ya nchi ya Urusi kuhusu kumaliza mzozo wa Syria kwa nchi hiyo kuteketeza silaha zake za kemikalia, wizara ya mambo ya nje imethibitisha.

Matangazo ya kibiashara

Taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya Iran imesema kuwa inaukubali mpango wa nchi ya Urusi kuhusu hatua za kuchukua kumaliza machafuko ya nchini Syria, ambapo ni kwakuifanya Serikali ya Syria kuteketeza silaha zake za kemikali.

Serikali ya Urusi hapo jana ilisema inawasiliana na utawala wa rais Assad kuangalia uwezekano wa taofa hilo kuziteketeza silaha zake za kemikali jambo ambalo hata hivyo lina nafasi ndogo ya kutekelezwa na utawala wa Syria.

Katika hatua nyingine rais wa Marekani, Barack Obama amesema iwapo Syria itakubali kuteketeza silaha zake za kemikali huenda hata nchi yake ikaachana na mpango wa kuishambulia kijeshi nchi hiyo.

Kwenye mahojiano maalumu ya televisheni, rais Obama amesema kuwa mpango huo huenda ukawa ni suluhu ya kumaliza machafuko ya nchini Syria kwakuwa utawala wa rais Assad umekuwa ukitumia silaha za kemikali dhidi ya raia.

Kauli ya raia Obama inakuja wakatu huu ambapo hiyo jana bunge la Congress liliahirisha kwa muda kujadili na kisha kupiga kura kuamua hatma ya nchi hiyo kuivamia kijeshi nchi ya Syria au lah.

Urusi imekuwa mstari wa mbele kupinga hatua zozote za kijeshi kuchukuliwa dhidi ya Syria ikisema kufanya hivyo kutaharibu hali ya usalama kwenye eneo la mashariki ya kati na pia kutachangia kukithiri kwa vitendo vya kigaidi.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi, Sergei Lavrov ameiomba nchi ya Syria kuruhusu silaha zake kuwa chini ya unagalizi wa idara za kimataifa ya silaha za kemikali na kuruhusu ziharibiwe.