ICC-KENYA

Naibu wa rais wa Kenya, William Ruto na mwandishi wa habari Joshua Arap San'g wakana mashtaka yanayowakabili kwenye mahakama ya ICC

Naibu wa rais wa Kenya, William Ruto akiwa kwenye mahakama ya ICC mjini The Hague
Naibu wa rais wa Kenya, William Ruto akiwa kwenye mahakama ya ICC mjini The Hague Reuters

Kesi ya uhalifu dhidi ya binadamu inayomkabili naibi wa rais wa Kenya, William Ruto na mwandishi wa habari, Joshua Arap San'g imeanza mjini The Hague, Uholanzi ambapo wote wawili wamekana kuhusika na makosa yanayowakabili.

Matangazo ya kibiashara

Mwendesha mashataka mkuu wa mahakama ya ICC, Fatou Bensouda alianza kwa kueleza namna watuhumiwa wote wawili walivyoshiriki kutekelea uhalifu dhidi ya binadamu wakati wa vurugu za uchaguzi mkuu wa mwaka 2007-2008.

William Ruto na Joshua San'g wanakabiliwa na makosa ya uhalifu dhidi ya binadamu, makosa wanayodaiwa kuyatenda wakati wa vurugu za uchaguzi mkuu wa mwaka 2007-2008 ambapo watu wanaokadiriwa elfu 1 walipoteza maisha na wengine zaidi ya laki sita wakiopoteza makazi yao.

Ruto aliwasili mjini The Hague siku ya Jumatatu tayari kuanza kusikiliza kesi dhidi yake hii leo kwenye mahakama ya ICC.

Kesi hiyo inaanza kuunguruma hii leo huku zikiwa zimepita siku chache tu toka wabunge nchini humo wapige kura na kupitisha muswada unaoitaka nchi hiyo kujiondoa kwenye mkataba wa Roma na kutoitambua mahakama hiyo.

Hata hivyo hatua hiyo ya wabunge haitaathiri kwa vyovyote mwenendo wa kesi inayomkabili naibu wa rais William Ruto kwakuwa ili mchakato huo uweze kufanikiwa ni lazima pia upigiwe kura kwenye baraza la Umoja wa Mataifa na kisha baadae mwaka mmoja ndipo mchakato wa kuiondoa Kenya uanze.

Naibu wa rais William Ruto na mwenzake Joshua Arap San'g wote kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka matatu ya mauaji, kuwafukuza watu na mateso dhidi ya raia, watuhumiwa wote wawili wanatarajiwa kukana mashtaka yao.

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta nae anakabiliwa na mashtaka kama hayo kwenye mahakama hiyo ya ICC na kesi zake zinatarajiwa kuanza kutimua vumbi mnamo tarehe 12 ya mwezi November mwaka huu.

Mamia ya wabunge wa Kenya wako mjini The Hague kumuunga mkono naibu wa rais William Ruto.

Vurugu za mwaka 2007-2008 zinaelezwa kuchochewa na ukabila vurugu zinazodaiwa kutekelezwa kwa sehemu kubwa na kabila la wakikuyu ambao wanaelezwa kuwa walikuwa ni wanamuunga mkono rais aliyemaliza muda wake, Mwai Kibaki.