Mapigano zaidi yashuhudiwa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, 60 waripotiwa kuuawa
Imechapishwa: Imehaririwa:
Wanajeshi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wanaendelea kukabiliana na kundi la wanajeshi watiifu kwa rais aliyepinduliwa madarakani, Francois Bozize, mapigano ambayo mpaka sasa yamesababisha vifo vya watu 60.
Mapigano haya makubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa toka kufanyika kwa mapinduzi ya kijeshi nchini humo, yamefanyika kwenye mji wa Bossangoa mji ulioko kilometa 250 toka mji mkuu wa taifa hilo Bangui.
Mji huo ambao ulikuwa ni makazi ya rais Bozize aliyeongoza taifa hilo kwa zaidi ya miaka kumi kabla ya kupinduliwa madarakani na waasi wa Seleka miezi sita iliyopita kumeshuhudiwa maelfu ya wananchi wakiyakimbia makazi yao.
Msemaji wa rais Michel Djotodia, Guy-Simplice Kodegue amethibitisha kutokea kwa mapigano ambayo anadai wapiganaji watiifu kwa rais Bozize walijipenyeza kwenye mji huo na kuanza kuharibu madaraja na miundo mbinu mingine mapigano yanayokuja kama ulipizaji kisasi kwa waislamu walio wengi kwenye mji huo.
Djotodia ambaye aliapishwa mwezi mmoja uliopita mjini Bangui, anakuwa rais wa kwanza wa madhehebu ya Waislamu, jambo ambalo linahusishwa na kuzuka kwa mapigano haya.
Siku ya Jumatatu na usiku wa kuamkia leo, kumesikika milio ya risasi na mabomu kwenye mji wa Bouca barabara inayoelekea Bossangoa ambako mauaji hayo yametokea.
Mashirika ya kutetea haki za bunadamu nchini humo yametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuingilia kati machafuko yanayoshuhudiwa nchini humo.
Waasi wa Seleka nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati toka waingie madarakani wamekuwa wakishutumiwa na Umoja wa Mataifa kutekeleza vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu.