CONGO BRAZAVILLE

Wanajeshi sita wahukumiwa kifungo nchini Congo Brazaville kwa kuhusika na ulipuaji wa ghala la silaha

Le site de Mpila, au Congo-Brazzaville, après le drame.
Le site de Mpila, au Congo-Brazzaville, après le drame. Reuters

Mahakama kuu nchini Congo Brazaville imewakuta na hatia wanajeshi sita na kuwahukumu kifungo jela huku ikiwaachia huru watu wengine zaidi ya 26 ambao kwa pamoja walikuwa wanatuhumiwa kulipua ghala la silaha mwaka 2012.

Matangazo ya kibiashara

March 4 mwaka 2012 kulitokea mlipuko mkubwa kwenye ghala la silaha mjini Brazaville na kusababisha vifo vya watu zaidi ya mia tatu huku wengine zaidi ya elfu mbili na mia tatu wakijeruhiwa na wengine elfu kumi na saba wakipoteza makazi yao.

Tukio hilo la mlipuko wa ghala la silaha lilikuwa ni baya zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini humo ambapo Serikali iliunda tume maalumu ya uchunguzi kubaini chanzo cha mlipuko huo.

Hii leo majaji waliokuwa wanasikiliza kesi hiyo wakati wakisoma hukumu yao, wamesema kuwa wameridhishwa na ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka ambao ulithibitisha wanajeshi hao sita kuhusika moja kwa moja na njama za kulipua ghala hilo.

Mtuhumiwa mkuu kwenye kesi hiyo, Koplo Kakom Kouack Blood alipatikana na hatia ya makosa ya kutekeleza makusudi tukio la kuwasha moto kwenye chumba cha kuhifadhia silaha mjini Mpila na kuhukumiwa kifungo cha miaka 15 jela sambamba na kazi ngumu.

Mahakama hiyo pia imemkuta na hatia aliyekuwa naibu wa usalama wa taifa nchini humo na kumuhukumu kifungo cha miaka mitano jela na kulipa faini ya euro elfu 18 baada ya kupatikana pia na makosa mengine ya matumizi mabaya ya ofisi.

Wengine waliohukumiwa kwenye kesi hiyo ni makamishna wa polisi ambao wote kwa pamoja wamehukumiwa kifungo cha miaka miwili jela na kutakiwa kila mmoja kulipa faini ya euro 304.

Jaji wa mahakama hiyo, Mathurin Bayi ametoa onyo kwa maofisa wengine wa polisi huku akitangaza kuwaachia huru watuhumiwa wengine zaidi ya 26 waliokuwa wamejumuishwa kwenye kesi hiyo.