KOREA KUSINI-KOREA KASKAZINI

Korea Kusini na Korea Kaskazini zakubaliana kuanza uzalishaji kwenye kiwanda cha Kaesong

Nchi za Korea Kusini na Korea Kaskazini hii leo zimekubaliana kwa pamoja kufungua shughuli za kiwanda cha pamoja cha Kaesong kwa muda kuanzia Jumatatau ya wiki ijayo baada ya kuwa kimefungwa kwa zaidi ya miezi mitano.

Viongozi wa Korea Kusini na Kaskazini wakikabidhiana nyaraka hivi karibuni baada ya kufikia muafaka
Viongozi wa Korea Kusini na Kaskazini wakikabidhiana nyaraka hivi karibuni baada ya kufikia muafaka REUTERS/Korea Pool/News1
Matangazo ya kibiashara

Kufunguliwa kwa kiwanda hiki cha pamoja kati ya mataifa hayo mawili, kuna kuja kufuatia mazungumzo ya muda mrefu kati ya nchi hizo mbili kuhusu uendeshaji wa kiwanda hicho ambacho kinategemewa na pande hizo mbili.

Kutangazwa kwa tarehe rasmi ya kuanza kwa shughuli za kiwanda hicho kumepokelewa kwa mikono miwili na wachambuzi wa masuala ya siasa ambao wanaona kuwa hatua hiyo itaimarisha uhusiano wa kimipaka baina ya mataifa hayo mawili.

Waziri mmoja wa Korea Kusini amenukuliwa na vyombo vya habari akidai kuwa mpango madhubuti wa kukifanya kiwanda hicho kishindane kwenye soko la kimataifa tayari imeandaliwa na kwamba wanaimani kuwa mpango wao utafanikiwa.

Wachambuzi wa masuala ya uchumi wanasema kuwa kufunguliwa kwa shughuli za uzalishaji kwenye kiwanda cha Kaesong kutatoa nafasi kwa nchi hiyo mbili kuanza tena biashara ya ushirikiano itakayosaidia kuimarisha uchumi wa mataifa haya.

Mwezi mmoja uliopita viongozi wa Korea Kusini na Korea Kaskazini walikutana kwa mazunguzmo yaliyolenga kumaliza tofauti zao na kuanza uzalishaji upya kwenye kiwanda hicho baada ya shughuli zake kusimama kwa zaidi ya miezi mitano.

Mwezi April mwaka huu Serikali ya Pyongyang ilipiga marufuku wafanyakazi wa Korea Kusini kuingia nchini humo kufanya kazi kwenye kiwanda hicho ambapo baadae nchi hiyo ikaamua kuwarudisha nyumbani zaidi ya wafanyakazi elfu 53 wa Korea Kusini.