LIBYA

Kumetokea mlipuko mkubwa wa bomu nje ya ofisi za wizara ya mambo ya nje ya Libya mjini Benghazi

Kumetokea mlipuko mkubwa wa bomu nje ya ofisi za wizara ya mambo ya nchi za nje ya Libya kwenye mji wa Benghaz ambapo majengo kadhaa pia yameharibiwa kutokana na mlipuko huo, watu walioshuhudia tukio hilo wamesema.

Moja ya mashambulizi ya bomu la kutegwa kwenye gari yaliyotekelezwa hivi karibuni mjini Benghazi, Libya
Moja ya mashambulizi ya bomu la kutegwa kwenye gari yaliyotekelezwa hivi karibuni mjini Benghazi, Libya Reuters
Matangazo ya kibiashara

Shambulio hili la bomu kwenye ofisi za wizara ya mambo ya nje ya Libya linatekelezwa ikiwa ni mwaka mmoja umepita toka makundi ya kigaidi nchini humo yaushambulie ubalozi wa Marekani mjini humo na kuwauwa maofisa wa nne wa ubalozi akiwemo balozi wake.

Ingawa taarifa hizo zimethibitishwa na vyombo vya usalama mjini Benghazi, bado haijafahamika haswa chanzo cha mlipuko huo ingawa watu walioshuhudia tukio hilo wanadai kuwa bomu hilo lilitegwa kwenye gari.

Hakuna taarifa zozote rasmi zilizotolewa kuhusu vifo ama kuwepo kwa majeruhi kwenye tukio hilo ingawa majengo mengi jirani na jengo hilo yameharibiwa kutokana mlipuko.

Mpiga picha wa kituo cha Ufaransa cha AFP amesema sehmu kubwa ya jengo la jeshi la Libya limeharibiwa ikiwemo pia majengo ya kituo cha polisi kilichoko kwenye eneo hilo.

Mji wa Beghazi toka kuangushwa na kuuawa kwa mtawala wa zamani wa taifa hilo Kanali Muamar Gaddafi mji huo umekuwa ukishuhudia mashambulizi ya mara kwa mara yanayodaiwa kutekelezwa na wafuasi wa kiongozi huyo wa zamani wa Libya.

Mashambulizi mengi kwenye mji ho yamekuwa yakilenga ofisi za mashirika ya mataifa ya magharibi zikiwemo balozi za Marekani, Uingereza na Ufaransa ambazo nchi zao zilishiriki katika vita vya kuung'oa utawala wa Gaddafi.