MAREKANI-SYRIA-URUSI

Obama: Tunasitisha kwa muda upigaji kura kuidhinisha mpango wa kijeshi dhidi ya Syria

Rais wa Marekani, Barack Obama hapo jana ametangaza kuahirisha mpango wa nchi yake kuishambulia kijeshi nchi ya Syria baada ya utawala wa rais Bashar al-Assad kusema uko tayari kutekeleza mpango wa Urusi wa kukusanya na kuteketeza silaha zake za kemikali.

Rais wa Marekani Barack Obama, akizungumza na waandishi wa habari kwenye ikulu yake mjini Washington
Rais wa Marekani Barack Obama, akizungumza na waandishi wa habari kwenye ikulu yake mjini Washington REUTERS/Jason Reed
Matangazo ya kibiashara

Akizungumza kwenye ikulu yake, rais Obama amewaambia wanahabari kuwa amewaomba wabunge kusitisha kwa muda mchakato wa upigaji kura kuidhinisha ama kutoidhinisha mpango wa Serikali yake kuishambulia kijeshi nchi ya Syria.

Rais Obama amesema kuwa kufanya hivyo kunaipa nafasi nchi yake kuendelea kufuatilia mchakato ulioanzishwa na Serikali ya Urusi ambayo imeitaka Serikali ya Syria kuzikusanya na kisha kuziteketeza silaha zake za kemikali.

Obama ameongeza kuwa hivi sasa atakuwa na mazungumzo ya karibu na rais wa Urusi, Vladmir Putin kuhusu mapendekezo ya nchi yake na atamtuma waziri wake wa mambo ya kugeni John Kerry kwenda nchini humo kukutana na mwenzake, Sergei Lavrov.

Kiongozi huyo amesema kuwa kwasasa ni vigumu kusema kuwa mpango huu utafanikiwa lakini nchi yake inatoa nafasi ya Serikali ya Assad kutekeleza kile ilichokiahidi na kuteketeza silaha zake za kemikali.

Hapo jana upinzani nchini Syria nao uliibuka na kupinga hatua ya Marekani kusitisha mpango wake wa kuishambulia kijeshi Syria kwa kile wapinzani wanadai kufanya hivyo kunatoa nafasi kwa wanajeshi wa Serikali kuwashambulia na kuzificha silaha za kemikali ambazo wanazo.

Serikali ya Syria kupitia kwa waziri wake wa mambo ya nje, Walid alMuallem amethibitisha nchi yake kukubaliana na wazo wa Urusi na tayari wanaanza mchakato wa kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa.