UFILIPINO

Wapiganaji wa kiislamu nchini Ufilipino wanaendelea kuwashikilia mateka raia zaidi ya 180

Wapiganaji wa kiislamu nchini Ufilipino wameendelea kutumia raia kama ngao yao dhidi ya mashambulizi ya wanajeshi wa Serikali kusini mwa nchi hiyo ambapo wanashikilia mateka watu zaidi ya 180.

Wakazi wa mji wa Zamboanga nchini Ufilipino wakikimbia mapigano kwenye mji wao kati ya waasi wa MNLF na wanajeshi wa Serikali
Wakazi wa mji wa Zamboanga nchini Ufilipino wakikimbia mapigano kwenye mji wao kati ya waasi wa MNLF na wanajeshi wa Serikali REUTERS/Erik De Castro
Matangazo ya kibiashara

Milio ya risasi imesikika kwenye mitaa ya mji wa Zamboanga ambako wapiganaji wa kundi la Moro National Liberation Front MNLF wanashikilia baadhi ya sehemu huku wakishinikiza kujumuishwa kwenye suluhu ya kitaifa pamoja na eneo hilo kujitenga.

Wapiganaji hao wametipotiwa kuchoma moto nyumba za wakaazi wa eneo hilo kama kitisho kwa wanajeshi wa Serikali kuingia kwenye maeneo ambayo wanayashikilia huku wakitumia pia walenga shabaha kuwarejesha nyuma wanajeshi wa Serikali.

Serikali ya Manila juma hili imetangaza kuanza operesheni ya kujaribu kuwaokoa watu wanaoshikiliwa mateka na wapiganaji hao baada ya juhudi za mazungumzo kati yao kugonga mwamba.

Taarifa za ndani toka kwenye kundi hilo zinasema kuwa hivi sasa wameiomba jumuiya ya kimataifa kuingilia kati mzozo unaoendelea kati yao na Serikali ili kupata suluhu na kusikilizwa kwa madai yao.

Kundi hili ambalo limejitenga toka kwenye makundi ya awali yaliyotiliana saini na Serikali kusitisha mapigano kusini mwa nchi hiyo limekuwa likiendesha uasi kwa muda sasa kabla ya mwishoni mwa juma kuvamia mji wa Zamboanga na kuua watu 16 pamoja na kuwashikilia wengine mateka.

Maelfu ya raia kwenye mji huo wameshuhudiwa wakiyakimbia makazi yao na kuomba hifadhi kwenye miji mingine wakati huu hofu zaidi ya kiusalama ikiendelea kutanda kwenye miji ya kusini mwa nchi hiyo.

Msemaji wa jeshi la Ufilipino, Luteni Kanali, Ramon Zagala amethibitisha kundi hilo la MNLF kuwashikilia mateka watu zaidi ya 180 na kuwatumia kama kinga yao dhidi ya mashambulizi ya wanajeshi wa serikali na hivyo wanashindwa kuingia kwenye eneo hilo wakihofia watu hao kuuawa.