EU

Bunge la Ulaya lapiga kura kuidhinisha benki kuu ya Umoja huo kuwa msimamizi mkuu wa benki zote za ukanda wa Ulaya

Wabunge wa bunge la Umoja wa Ulaya EU hii leo wamekubaliana kwa kauli moja kupitisha mpango wa awali ambao utairuhusu benki kuu ya Umoja huo kuwa mwangalizi mkuu wa mwenendo wa benki za nchi wanachama.

Wabunge wa bunge la Umoja wa Ulaya wakipiga kura kwenye moja ya mikutano yake
Wabunge wa bunge la Umoja wa Ulaya wakipiga kura kwenye moja ya mikutano yake europa.eu
Matangazo ya kibiashara

Mpango huu ambao ni hatua kubwa zaidi kuwahi kufikiwa na wabunge wa Ulaya unalenga kuhakikisha kunakuwa na uangalizi wa karibu kuhusu mwenendo wa benki za nchi wanachama ili kuzuia kuwa na matumizi makubwa.

Hatua hii inakuja kufuatia nchi nyingi ambao ni wanachama wa Umoja wa Ulaya kuingia kwenye mdororo wa uchumi kutokana na kukosekana kwa mfumo mmoja ambao ungehakikisha unasimamia huduma za kifedha zinazofanyika kwenye benki za nchi wanachama.

Wataalamu wa masuala ya uchumi wanasema kuwa matatizo ya kiuchumi yaliyozikumba baadhi ya nchi za ukanda wa Ulaya yalitokana na benki zao kuwa na matumizi makubwa pamoja na kukosekana kwa mfumo wa kusimamia uhamishaji wa fedha kutoka akaunti moja kwenda nyingine.

Makubaliano haya ya mwanzo yaliungwa mkono kwa kura 556 kati ya 54 ambazo zilisema hapa kuhusu kuiidhinisha benki kuu ya Umoja wa Ulaya kuwa msimamizi mkuu wa benki zote za nchi wanachama kuhakikisha kunakuwa na matumizi sahihi ya fedha.

Wabunge hao pia juma hili waliahirisha kupigia kura muswada mwingine wa kuidhinisha bodi ya udhamini ya chombo kitakachokuwa na jukumu la kufanya ukaguzi kwenye benki za umoja huo mpaka pale kamati maalumu itakapoundwa ambayo itakuwa na mwenyekiti na kaimu mwenyekiti.

Akizungumzia uamuzi uliofanywa na wabunge, mkuu wa tume ya Umoja wa Ulaya, Jose Manuel Barosso amesema hii ni hatua muhimu kufikiwa na nchi wanachama na imekuja wakati muafaka kunusuru uchumi wa mataifa hayo.

Mpango huu utatakiwa kuanza kufanya kazi ndani ya mwaka mmoja ambapo benki kuu ya Umoja wa Ulaya itapewa jukumu la kusimamia sera na matumizi ya fedha kwenye benki za nchi wanachama pamoja na kutunga sheria za fedha kuzuia fedha chafu.