GENEVA-URUSI-MAREKANI-SYRIA

Mawaziri wa mambo ya kigeni wa Marekani na Urusi wanakutana mjini Geneva, Uswis kujadili mzozo wa Syria

Mawaziri wa mambo ya kigeni wa Urusi na Marekani wanakutana mjini Geneva, Uswis hii leo kujadili mpango uliopendekezwa na nchi ya Urusi kuhusu utawala wa Syria kuteketeza silaha zake za kemikali.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi, Sergei Lavrov(kushoto) akiwa na mwenzake wa Marekani, John Kerry(kulia) viongozi hawa wanakutana mjini Geneva hii leo
Waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi, Sergei Lavrov(kushoto) akiwa na mwenzake wa Marekani, John Kerry(kulia) viongozi hawa wanakutana mjini Geneva hii leo Reuters
Matangazo ya kibiashara

Mawaziri hao John Kerry wa Marekani na mwenzake wa Urusi, Sergei Lavrov wanakutana mjini Geneva, Uswis hii leo tayari kwa mazungumzo ya ana kwa ana kuhusu namna ya kuhakikisha Syria inasalimisha silaha zake za kemikali kwa jumuiya ya kimataifa.

Tayari waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, John Kerry amewasili mjini Geneva tayari kwa mazungumzo hayo ambayo kwa sehemu kubwa yametokana na msimamo wa Urusi kuhusu hatua za kuchukua kumaliza mzozo wa Syria.

Wakati akiondoka mjini Moscow, Urusi kuelekea nchini Uswis, waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi, Sergei Lavrov amewaambia wanahabari kuwa yeye na mwenzake wanatarajia kuwa na mjadala wa kina kuhusu mapendekezo ya Urusi na namna bora ya kushughulikia suala hilo.

Hivi karibuni rais wa Urusi, Vladmir Putin alitaka mawaziri hao wakutane kuzungumzia mgogoro wa Syria mazungumzo ambayo hata hivyo yalikuwa kwenye hati hati ya kutofanyika baada ya upande mmoja nchini Syria kudaiwa kutumia silaha za kemikali huku Marekani ikisisitiza inaushahidi kuwa ni utawala wa rais Assad.

Mazungumzo ya hii leo yanalenga kutathimini mapendekezo ya Urusi ambayo imetaka kuchukuliwa kwa hatua nne muhimu kuhakikisha utawala wa rais Bashar al-Assad unakusanya na kuonyesha maghala yote ambayo unahifadhi silaha za kemikali.

Wachambuzi wa mambo wanaona kuwa licha ya mapendekezo hayo ya Urusi huenda mazungumzo ya hii leo yasifue dafu kwakuwa Marekani inaenda huku ikitaka kuchukuliwa kwa hatua kali dhidi ya Syria na kwa upande mwingine Serikali ya Urusi ikitaka diplomasia itumike zaidi.