KAMPALA-DRC-M23

Mazungumzo ya Kampala kati ya Serikali ya DRC na kundi la waasi wa M23 yaendelea

Baadhi ya wajumbe ambao wanahudhuria mazungumzo ya Kampala kati ya M23 na serikali ya DRC
Baadhi ya wajumbe ambao wanahudhuria mazungumzo ya Kampala kati ya M23 na serikali ya DRC Reuters

Mazungumzo ya amani kati ya waasi wa M23 na Serikali ya DRc yameingia kwenye siku yake ya tatu mjini Kampala, Uganda huku wajumbe wa pande zote mbili wakionesha matumaini ya kufikia muafaka.

Matangazo ya kibiashara

Mwandishi wetu wa Kampala, Tonny Singoro anasema kuwa mazungumzo ya pande hizo mbili yameingia kwenye siku yake ya tatu mfululizo hii leo huku kila upande ukiwa na matumaini ya kufikia muafaka ndani ya siku 14.

Ujumbe wa kundi la waasi wa M23 kwenye mazungumzo hayo, wamemwambia mwandishi wetu kuwa wao wako tayari na watahakikisha kuwa wanafikia muafaka ndani ya siku kumi na nne kama walivyoagizwa na viongozi wa nchi za maziwa makuu.

Kiongozi wa Ujumbe wa M23 kwenye mazungumzo hayo, Rene Abandi ameiambia rfikiswahili kuwa, wao watahakikisha wanafanikisha mazungumzo ya safri hii na kusalimisha silaha zao pale Serikali ya Kinshasa itakapotekeleza matakwa yao.

Kabla ya kuanza kwa mazungumzo hayo, waasi wa M23 wametaka kundi la FDLR lililoko nchini DRC lifurushwe pamoja na kuhakikisha wakimbizi wa nchi hiyo walioko nchini Rwanda na Burundi wanaejea nyumbani.

Kwa upande wa ujumbe wa Serikali ya DRC, kiongozi wa msafara hup, Francosi Mwamba amesisitiza utayari wao wa kufikia muafaka na waasi hao na kuongeza kuwa watatekeleza kile walichoagizwa na viongozi wa nchi za maziwa makuu.

Mazungumzo haya yanafanyika kufuatia maagizo ya viongozi wa nchi za Maziwa makuu baada ya mkutano wao wa juma lililopita ambapo walitoa siku 14 kwa pande hizo mbili kumaliza tofauti zao.