UHOLANZI-INDONESIA

Uholanzi yaomba radhi kwa nchi ya Indonesia kwa mauaji yaliyofanywa na wanajeshi wake

Askari wa Uholanzi akiwa na mateka raia wa Indonesia wakati wa ukoloni
Askari wa Uholanzi akiwa na mateka raia wa Indonesia wakati wa ukoloni Dutch gvt

Katika kile kinachoonekana ni kutaka kumaliza chuki biana yake na nchi ya Indonesia, Serikali ya Uholanzi kwa mara ya kwanza imeomba radhi hadharani kwa wananchi wa Indonesia kutokana na mauaji yaliyofanywa na wanajeshi wake kwenye miaka ya 1940.

Matangazo ya kibiashara

Wanajeshi wa Uholanzi wanatuhumiwa kutekeleza mauaji hayo huku familia za watu waliokuwa wamekamatwa na wanajeshi hao wakishuhudia ndugu zao wakiuawa kwa risasi.

Kauli ya Uholanzi ni ya kwanza kutolewa hadharani kufuatia miongo kadhaa ya madai ya Serikali ya Indonesia ikitaka nchi hiyo iombe radhi na kulipa fidia kwa wanafamilia ambao walipoteza ndugu zao.

Msamaha huo wa wazi umeombwa na balozi wa Uholanzi nchini Indonesia, Tjeerd De Zwaan wakati wa hafla iliyofanyika mjini Jakarta kwenye ubalozi wa Uholanzi akiomba radhi kwa niaba ya Serikali yake.

Balozi Zwaan amesema kuwa anatumaini kuwa msamaha huu utaponya vidonda vya wanafamilia waliopoteza ndugu zao kati ya mwaka 195 na 1949 ambapo wanajeshi wake walitumia nguvu kubwa dhidi ya raia.

Mwezi mmoja uliopita Serikali ya Uholanzi ilitangaza kulipa kiasi cha euro elfu 20 kwa wake na wanafamilia ambao walipoteza ndugu zao wakati wa utawala wa kikoloni ambapo taifa hilo lilitawaliwa na Uholanzi.

Hatua hii inakuja huku mwezi August mwaka huu ikiwalipa wanawake kumi ambao walikuwa ni wake waliopoteza waume zao kati ya mwaka 1945/ 1947 ambapo watoto wao walikuwa sehemu ya sherehe iliyoandaliwa na ubalozi wa Uholanzi nchini Indonesia.