MALI

Wanajeshi 3 wa Serikali ya Mali wajeruhiwa baada ya makabiliano na waasi wa Tuareg kaskazini mwa nchi hiyo

Wapiganaji wa kundi la Tuareg nchini Mali
Wapiganaji wa kundi la Tuareg nchini Mali REUTERS/Cheick Diouara

Wanajeshi watatu wa jeshi la Mali wamejeruhiwa kwenye makabiliano na kundi la waasi wa Tuareg, mapigano yanayozuka ikiwa imepita miezi kadhaa toka pande hizo mbili zitiliane saini kusitisha vita kaskazini mwa nchi hiyo.

Matangazo ya kibiashara

Jeshi la Mali limethibitisha kutoke kaw mapigano hayo kwenye mji wa Lere ambako inadaiwa kuwa waasi wa Tuareg wamekuwa wakiendesha operesheni kwa kushirikiana na wapiganaji wa kundi la kigaidi la Al-Qaeda.

Mapiganao haya yanakuja ikiwa yamepita majuma kadhaa toka rais mpya wa Mali, Ibrahim Boubacar Keita aapishwe kuchukua madaraka toka kwenye Serikali ya mpito na kuahidi kuiunganisha nchi yake.

Waasi wa kundi la Tuareg walibeba silaha toka mwaka 1960 lakini walikuwa hawana nguvu mpaka kufikia mwaka jana ambapo walifanikiwa kuchukua miji mingi kaskazini mwa nchi hiyo wakitaka kujitenga.

Vikosi vya Umoja wa Afrika AU vinaendelea kuimarisha usalama kaskazini mwa nchi hiyo wakati huu ambapo wanajeshi wa Ufaransa wameanza kuondoka nchini humo baada ya kufanikiwa kuwafurusha wapiganaji hao.

Msemaji wa jeshi la Mali, Kapteni Modibo Naman Traore amesema kuwa waasi hao wakiwa kwenye gari la wazi walisimamishwa na wanajeshi wa Serikali lakini walikataa kutii amri na kuanza kuwashambulia kwa risasi.

Kiongozi wa kundi hilo Attaye Mohamed amewatuhumu wanajeshi wa Serikali kwa kuanza kuwashambulia wapiganaji wake akidai kuwa waliwazingira kwenye ngome zao kwa lengo la kutaka kuwashambulia na ndipo walipojihami.

Mwezi June mwaka huu waasi wa Tuareg walitia saini ya kusitisha vita kaskazini mwa nchi hiyo chini ya uangalizi wa rais wa Bukina Faso, Blaise Compaore kabla ya nchi hiyo kufanya uchaguzi wake mkuu.

Licha ya makubaliano hayo, bado kumeendelea kushuhudiwa mapigano kwenye baadhi ya miji kaskazini mwa nchi hiyo hasa kwenye mji wa Kidal ambako ilikuwa ngome kuu ya wapiganaji hao.