Kiyonga: MONUSCO hawapaswi kuendelea na operesheni yoyote ya kijeshi mashariki mwa DRC
Mazungumzo kati ya M23 na Serikali ya Kinshasa yameendelea mjini Kampala huku wito ukitolewa kwa wanajeshi wa vikosi vya MONUSCO vilivyoko mashariki mwa DRC kutofanya mashambulizi yoyote kwa wakati huu.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Kauli hii imetolewa na mratibu wa mazungumzo ya Kampala, Crispus Kiyonga ambaye pia ni waziri wa ulinzi wa taifa hilo ambaye ametaka vikosi vya MONUSCO kutotekeleza operesheni yoyote mashariki mwa nchi hiyo.
Kauli ya Kiyonga inakuja kufuatia kuwepo taarifa kuwa wanajeshi wa MONUSCO na wale wa vikosi maalumu vya Umoja wa Mataifa wanapanga kuendeleza mashambulizi zaidi kuwafurusha wapiganaji wa kundi la M23.
Waziri Kiyonga amevitaka vikosi hivyo kusitisha operesheni zozote za kijeshi wala kuwalazimisha wapiganaji wa M23 kusalimisha silaha kama azimio la Umoja wa Mataifa linavyotaka.
Vikosi vya UN nchini humo vimekosolewa vikali na wananchi wa Goma, ambao wanaona hakuna haja ya vikosi hivyo kusitisha operesheni zake licha ya mazungumzo yanayofanyika mjini Kampala.
Juma moja lililopita viongozi wa nchi 11 za ukanda wa maziwa makuu walitoa siku 14 kwa pande hizo mbili kusitisha vita na kurejea kwenye meza ya mazungumzo kujaribu kimaliza mzozo uliopo.
Kundi la M23 linataka waasi wa FDLR kutoka Rwanda wadhibitiwe pamoja na kurejea nyumbani kwa wakimbizi wa DRC ambao wako nchini Rwanda na Uganda.