AFGHANISTAN

Taliban wafanya shambulio la bomu nje ya ubalozi wa Marekani nchini Afghanistan

Watu wenye silaha wamevamia na kushambulia ubalozi wa Marekani ulioko kwenye eneo la Herat nchini Afghanistan mapema asubuhi ya hii leo na kushuhudia makabiliano makali ya risasi kati ya wanajeshi wa Marekani na wapiganaji hao. 

Askari wa Afghanistan wakijaribu kumuokoa mmoja wa majeruhi kwenye shambulio la leo asubuhi nje ya ubalozi wa Marekani mjini Herat
Askari wa Afghanistan wakijaribu kumuokoa mmoja wa majeruhi kwenye shambulio la leo asubuhi nje ya ubalozi wa Marekani mjini Herat Reuters
Matangazo ya kibiashara

Taarifa ya polisi nchini humo inasema kuwa watu hao wenye silaha wakiwa na mtu mwingine aliyevalia milipuko akiwa kwenye gari moja alijilipua nje kidogo ya ubalozi huo na kusababisha uharibifu mkubwa.

Hata hivyo wizara ya mambo ya nje ya Marekani imetoa taarifa kupitia mtandao wa Twitter ukikanusha maofisa wake wa ubalozi kujeruhiwa kwenye shambulio hilo lililotekelezwa asubuhi wakati wafanyakazi wake wakiingia kazini.

Polisi nchini Afghanistan wamesema kuwa katika shambulio hilo mtu mmoja ndiye ameripotiwa kupoteza maisha huku wengine zaidi ya kumi na nane wakijeruhiwa kutokana na mlipuko wa bomu.

Tayari kundi la wanamgambo wa Taliban nchini humo limekiri kuhusika na shambulio hilo na kuongeza kuwa limeleta madhara makubwa kwa wafanyakazi wa ubalozi wa Marekani na polisi wa Afghanistan.

Askari wa nne wa Afghanistan ni miongoni mwa wale waliojeruhiwa kwenye shambulio hilo ambalo limeacha lango kuu la kuingia kwenye ubalizi huo ukiwa umeharibika vibaya.

Serikali ya Marekani inasema kuwa mtu aliyejitoa muhanga alilenga kujipenyeza na kuingia ndani ya ubalozi huo lakini baada ya kudhibitiwa alianza kufyatua risasi kabla ya kujilipua.