Baraza la kitaifa la upinzani nchini Syria lasema litahudhuria mazungumzo ya amani mjini Geneva

Baraza la kitaifa la upinzani nchini Syria, limetangaza kushiriki mazungumzo ya amani ya mjini Geneva kwa masharti kwamba baadhi ya madai yao yatekelezwe kabla hawajashiriki mazungumzo hayo.

Baadhi ya viongozi wa baraza la kitaifa la upinzani nchini Syria wanaokutana mjini, Instanbul
Baadhi ya viongozi wa baraza la kitaifa la upinzani nchini Syria wanaokutana mjini, Instanbul Reuters
Matangazo ya kibiashara

Kwenye taarifa yao waliyoitoa hii leo mjini Instanbul, Uturuki, baraza hilo linataka mambo kadhaa kwanza yatekelezwe na utawala wa Syria ndipo wao washiriki mazungumzo ya amani yaliyopangwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu ama mwakani.

Taarifa yao inataka kwanza kuwepo na hakiksho la kupatikana kwa Serikali ya kitaifa mara baada ya mazungumzo hayo, pili mashirika ya misaada ya Umoja wa Mataifa yaruhusiwe kwenda kwenye maeneo ya watu wanaohitaji, na tayu kuachiliwa huru kwa wafungwa wa kisiasa.

Baraza hilo pia linataka makundi mengine ya waasi yanayopigana nchini Syria kushiriki kwenye mazungumzo hayo kwakuwa lengo ni kutaka kupata umoja wa kitaifa kuushinda utawala wa rais Bashar al-Asad.

Kauli hii ya upinzani inatolewa wakati huu ambapo kunashuhudiwa mgawanyiko mkubwa ndani ya upinzani nchini Syria, ambapo kuna makundi yanayounga mkono mazungumzo ya Mjini Geneva na wengine hawaungi mkono.

Serikali ya Urusi ambayo ni mmoja wa waandaaji wa mkutano huo imeshatangaza wazi kuwa hakuna kuwepo kwa masharti yoyote kabla ya kufanyika kwa mazungumzo hayo.