SYRIA-UTURUKI

Waasi nchini Syria waunda Serikali ya mpito kutawala maeneo wanayoyashikilia

Baadhi ya viongozi wa muungano wa kitaifa wa waasi nchini Syria wanaokutana mjini Instanbul
Baadhi ya viongozi wa muungano wa kitaifa wa waasi nchini Syria wanaokutana mjini Instanbul Reuters

Muungano wa waasi wa Syria wanaotambuliwa kimataifa, wamekubaliana kwa kauli moja kuwa na Serikali yao ya mpito ambayo itakuwa inasimamia shughuli za kwenye maeneo ambayo wanayashikilia ndani ya Syria.

Matangazo ya kibiashara

Kwenye mkutano wao unaoendelea mjini Instanbul Uturuki, ujumbe wa baraza la kitaifa la muungano wa waasi wa Syria, wamekubaliana kuteua viongozi ambao watakuwa mawaziri kwenye Serikali ya mpito kwaajili ya kusimamia shughuli za maeneo ambayo wanayakalia nchini humo.

Uamuzi huu unakuja saa chache baada ya hapo jana, baraza hilo kukubaliana kimsingi kwamba watahudhuria mazungumzo ya mjini Geneva kwa masharti ambayo ni lazima yatekelezwe kabla ya wao kushiriki.

Kwenye makubaliano yao, ujumbe wao pia umesisitiza kuwa kwenye Serikali yao ya mpito rais Asad hatakuwa na ushiriki wowote kama sharti mojawapo la wao pia kushiriki kwenye mazungumzo ya kampala.

Hata hivyo wakati wakikubaliana kuwa na Serikali kwenye maeneo ambayo wanayashikilia, hii leo na jana majeshi ya Serikali yameanza operesheni kwenye mji wa Allepo na Homs kujaribu kuirejesha kwenye himaya yao baadhi ya miji ambayo inakaliwa na waasi.

Ndege za jeshi la Syria zimeripotiwa usiku wa kuamkia hii leo kushambulia sehemu ya mji wa Allepo kuwakabili makundi ya waasi ambayo yamekuwa yakiendesha harakati zao.

Wakati haya yote yanajiri tayari kumeibuka mizengwe kuhusu kufanyika kwa mazungumzo ya mjini Geneva yanayosimamiwa na nchi za Marekani na Urusi huku upinzani ukieleza kuwa hautatambua ujumbe wa Iran ambao utajumuishwa kwenye mazungumzo hayo kwakuwa ni washirika wa utawala wa rais Asad.