SRI LANKA

Kuelekea mkutano wa Jumuiya ya Madola, Sri Lanka yasema haina chakuficha kuhusu suala la haki za binadamu

Rais wa Sri Lanka, Mahinda Rajapakse
Rais wa Sri Lanka, Mahinda Rajapakse Reuters

Rais wa Sri Lanka, Mahinda Rajapaksa hii leo amejibu vikali tuhuma zilizoelekezwa dhidi ya nchi yake kuhusu uhalifu wa kivita, tuhuma ambazo huenda zikawa ajenda kuu ya mkutano wa Jumuiya ya madola unaotarajiwa kufanyika juma hili nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Rais, Rajapaksa amewaambia waandishi wa habari kuwa nchi yake haina jambo lolote la kuficha kuhusu tuhuma kwamba imekithiri kwa vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu pamoja na wanajeshi wake kushirikia vitendo vya uhalifu wa kivita wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchinu humo.

Kiongozi huyo ambaye atakuwa ni mwenyekiti wa mkutano wa siku tatu wa nchi wanachama za Jumuiya ya Madola, amesema yuko tayari kukabiliana kwa maneno na waziri mkuu wa Uingereza David Cameroon wakati wa mkutano huo lakini hatofanya hivyo kwa shinikizo.

Kauli ya rais Rajapaksa anaitoa wakati huu ambapo nchi za Canada, India na Mauritius zimesema hazitawatuma mawaziri wake kuhudhuria mkutano huo kutokana na rekodi mbaya ya haki za binadamu ya nchi ya Sri Lanka.

Kiongozi huyo amejikuta kwenye shinikizo kubwa la Umoja wa Mataifa kufuatia hatua yake ya kukataa kupelekwa kwa jopo huru la uchunguzi nchini humo kuchunguza mauaji ya halaiki ya watu wa jamii ya Tamil wakati Serikali ilipokuwa ikikabiliana na waasi wa Tamil Tiger.

Zaidi ya raia elfu arobaini wa jamii ya Tamil waliuawa kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyokuwa vimedumu kwa zaidi ya miaka 39.