MISRI-URUSI

Lavrov na Shiogu wafanya ziara ya kihistoria nchini Misri, watangaza ushirikiano zaidi kati ya Urusi na Misri

Waziri wa mambo ya nje wa Urusi, Sergei Lavrov akiwa na ujumbe wake nchini Misri
Waziri wa mambo ya nje wa Urusi, Sergei Lavrov akiwa na ujumbe wake nchini Misri Reuters

Waziri wa Ulinzi wa Urusi akiambatana na waziri wa mambo ya kigeni wa nchi hiyo, hii leo wameendelea na ziara yao ya siku mbili nchini Misri, huku ujumbe wa pande zote mbili ukikubaliana kushirikiana kwenye mambo muhimu ya kiusalama, kisiasa na kiuchumi.

Matangazo ya kibiashara

Waziri wa Mambo ya kigeni wa Urusi, Sergei Lavrov na mwenzake wa Misri, Nabil Fahmy ndio walikuwa wa kwanza kuzungumza na waandishi wa habari asubuhi ya leo na kusisitiza kuwa wamezunguma mambo yote kuanzia sera ya mambo ya nje hadi masuala ya utalii.

Ziara ya viongozi wa Urusi nchini Misri inafanyika wakati huu ambapo hali ya kisiasa nchini humo hairidhishi huku jeshi likiunda Serikali ya mpito wakati huu ambapo rais Mohamed Morsi anaendelea kuwa kizuizini akisubiri kuanza kusikilizwa kwa kesi yake.

Kwenye ziara hiyo, ujumbe wa Urusi pia umemmjumuisha waziri wa ulinzi, Sergei Shoigu ambaye nae amekuwa na mazungumzo na mkuu wa majeshi ambaye pia ni waziri wa ulinzi Jenerali Abdel Fattah el-Sisi ambao nao wamekubaliana kushirikiana kwenye masuala ya usalama.

Shoigu anakuwa waziri wa kwanza wa ulinzi wa nchi ya Urusi kufanya ziara mjini Cairo toka mwaka 1971 siku chache kabla ya rais Anwar Sadat kujiondoa kwenye mkataba na utawala wa wakati huo wa Kisoviet na kuanza ushirikiana na nchi ya Marekani.

Duru za ndani kwenye ujumbe wa Urusi zimedokeza kuwa viongozi hao hawatatiliana saini mkataba wowote wa kijeshi wa kuiuzia silaha nchi hiyo kufuatia kile ambacho kimeendelea kushuhudiwa nchini humo.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa hivi karibuni, wananchi wengi w Misri wameonesha kuinga mkono zaidi nchi ya Urusi kuliko nchi ya Marekani kwa kile ambacho wanaamini zaidi kuliko nchi ya Marekani.

Wakati wa ziara ya viongozi wa Urusi nchini humo, picha za rais wa Urusi, Vladmir Putin zimeanza kuwa maarufu kwenye viunga vya jiji la Cairo na maeneo mengine kuonesha uungwaji mkono wake na wananchi.

Katika hatua nyingine viongozi hao wamekubaliana kuongeza juhudi zaidi katika kusaidia kupata suluhu ya mzozo wa Syria.