NELSON MANDELA

Rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini Mzee Nelson Mandela "Madiba" afariki dunia

Rais wa Afrika Kusini, Mzee Nelson Mandela "Madiba" 1918-2013
Rais wa Afrika Kusini, Mzee Nelson Mandela "Madiba" 1918-2013 Reuters

Rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini na aliyechaguliwa kidemokrasia, Mzee Nelson Mandela "Madiba" amefariki dunia hapo jana akiwa amezungukwa na familia yake mjini Johannesberg.

Matangazo ya kibiashara

Mandela amefariki dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu maradhi ya ini ambayo wakati fulani aliwahi kuugua wakati akiwa gerezani akitumikia kifungo kwa makosa ya kupigania haki ya watu weusi na ubaguzi wa rangi nchini mwake.

Aliyetangaza habari za kufariki kwa Mzee Nelson Mandela alikuwa ni rais wa taifa hilo, Jackob Zuma ambaye kwenye hotua yake amesema taiafa limepoteza baba na kiongozi aliyepigania haki za raia wote katika kuhakikisha mustakabali mwema wa wananchi wa Afrika Kusini.

Raid Zuma ameongeza kuwa kifo cha Mzee Mandela ni pigo sio tu kwa wananchi wa Afrika Kusini aliowatumikia wakati akiwa rais, bali ni kwa bara zima la afrika na dunia kwa ujumla.

Nelson Mandela amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 95 ambapo wakati wa sherehe za kumbukumbu yake ya kutimiza miaka hiyo alisherekea akiwa kwenye hospitali ya kijeshi ya mjini Johannesburg ambako alikuwa akipatiwa matibabu.

Mandela alitumikia kifungo cha maisha kwa miaka 27 kutokana na harakati zake za kupinga ubaguzi wa rangi na alifungwa katika kisiwa cha Robben na baadae kuachiwa huru mwaka 1990 ambapo alianzisha sera ya maridhiano.

Mwaka wa 1993 yeye pamoja na Frederik Willem de Klerk walitunukiwa tuzo ya amani ya Nobel kutokana na mchango wao katika harakati za kupigania haki za binadamu.

Maelfu ya raia wa Afrika Kusini wamekesha nje ya makazi yake ya mjini Soweto ambako amekuwa akiishi kwa kipindi cha maisha yake yote na hata wakati wa harakati za kupigania uhuru wa taifa lake.

Mbali na kutambulika kama mmoja wa watu waliohakikisha ubaguzi wa rangi unamalizika nchini Afrika Kusini, Mzee Madiba pia atakumbukwa kwa harakati zake za kupatanisha baadhi ya mataifa ya bara la Afrika kama vile mzozo wa Burundi na hata ule mgogoro wa Palestina na Israel.

Viongozi mbalimbali duniani wametuma salamu za rambirambi kwa raia wa Afrika Kusini na hasa rais Jackob Zuma huku kila anayetuma salamu hizo akimuelezea Mzee Madiba kwa namna alivyomfahamu wakati wa harakati zake.

Rais wa Marekani, Barack Obama, amesema kuwa dunia imepoteza mwanaharakati wa kweli na kiongozi shupavu aliyejitolea maisha yake yote kupigania uhuru wa raia wenzae wa Afrika Kusini waliokuwa wakinyanyaswa wakati wa ukoloni.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon kwa upande wake amemuelezea mzee Madiba kama moja ya viongozi wachache duniani waliokuwa na kipaji cha kusuluhisha hasa kwenye maeneo yaliyokuwa na mgogoro.