ICC-KENYA-UHURU KENYATTA

Mwendesha mashtaka wa ICC aomba kesi dhidi ya Kenyatta isogezwe mbele

Mwendesha mashtaka wa mahakama ya ICC, Fatou Bensouda
Mwendesha mashtaka wa mahakama ya ICC, Fatou Bensouda REUTERS/Michael Kooren

Mwendesha mashtaka mkuu kwenye mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ya ICC, Fatou Bensouda amewasilisha maombi rasmi kwa majaji wanaosikiliza kesi dhidi ya rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta kutaka kesi dhidi ya kiongozi huyo zisogezwe mbele. 

Matangazo ya kibiashara

Kwenye barua yake mwendesha mashtaka anataka kesi dhidi ya rais Kenyatta zisogezwe mbele zaidi ili kutoa nafasi kwa ofisi yake kukusanya ushahidi zaidi kufuatia shahidi muhimu kwenye kesi hiyo kutangaza kujiondoa.

Bensouda amesema kuwa kutokana na kujiondoa kwa shahidi muhimu kwenye kesi ya Kenyatta kumeifanya ofisi yake kuwa kwenye wakati mgumu wa kuanza kesi dhidi ya rais Kenyatta mwezi wa pili kama majaji wa mahakama hiyo walivyoamua kwakuwa shahidi muhimu amejiondoa.

Hatua hii ya mwendesha mashtaka imekuja siku chache toka yeye mwenyewe pamoja na jopo la waendesha mashtaka kwenye mahakama hiyo kutoa ripoti kwa majaji wa mahakama hiyo kuhusu kuingiliwa kwa mashahidi muhimu kwenye kesi hiyo pamoja na kutolewa kwa vitisho kwa mashahidi.

Bado majaji wa mahakama ya ICC hawajaamua iwapo watasogeza mbele kesi dhidi ya rais Kenyatta iliyopangwa kuunguruma mwezi wa pili hapo mwakani.

Wachambuzi wa mambo wanaona kuwa yale aliyokuwa akidai mwendesha mashtaka kuhusu kulindwa kwa mashahidi ynafaa yazingatiwe na majaji wa mahakama hiyo kwakuwa kujiondoa kwa mashahidi muhimu kwenye kesi hiyo kutaifanya kupoteza sifa za kuendelea.

Katika hatua nyingine wakosoaji wa kesi dhidi ya rais Kenyatta na naibu wake William Ruto wanasisitiza kuwa huku ni kushindwa kazi kwa ofisi ya mwendesha mashtaka na kwamba kesi hizi zitafikia tamati hata bila ya kusikilizwa zaidi kwakuwa hakuna ushahidi wa kutosha kuwashtaki viongozi hawa.

Hata hivyo mwendesha mashtaka amesema kuwa kutaka kusogezwa mbele kwa kesi dhidi ya Kenyatta hakumaanishi kuwa kesi dhidi ya naibu wake William Ruto nayo itasimama badala yake itaendelea kama ilivyokuwa imepangwa.