Kenya - Sheria

Majaji wa mahakama ya uhalifu wa kivita ya ICC kuamua kuhusu hatma ya Kesi ya rais wa Kenya Uhuru Kenyatta hii leo

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta REUTERS/Noor Khamis

Majaji wa mahakama ya kimataifa ya Uhalifu wa Kivita ya ICC, hii leo wanaketi kuamua hatma ya kesi ya tuhuma za kufadhili machafuko ya mara baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007/2008 nchini Kenya, inayomkabili rais wa taifa hilo Uhuru Mwigai Kenyatta.

Matangazo ya kibiashara

Kikao hichi kati ya upande wa Mashtaka na upande wa utetezi, kinafanyika kufuatia tarehe 23 ya mwezi january mwaka huu, ofisi ya mwendesha mashtaka kuwasilisha ombi kwenye mahakama hiyo kutaka kesi dhidi ya rais Kenyaata iliyokuwa imepangwa kuanza hii leo kusogezwa mbele kwa miezi mitatu zaidi.

Mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama hiyo, Fatou Bensouda amesema lengo la kutaka kuahirishwa kwa kesi hiyo ni kutokana na kuondolewa na kujiondoa kwa mashahidi muhimu kwenye kesi hiyo pamoja na kukosa ushirikiano toka Serikali ya Kenya na hivyo kutaka muda zaidi wa kukusanya ushahidi.

Uamuzi wa hii leo unasubiriwa kwa hamu, huku upande wa utetezi ukiwataka majaji wa mahakama hiyo, kutpilia mbali kesi dhidi ya mteja wao kwa madai kuwa ofisi ya mwendesha mashtaka haina ushahidi wa kutosha kuendelea na kesi dhidi ya rais Uhuru Kenyatta.

Rais Kenyatta anashtakiwa na mahakama ya ICC kwa kuhusika kufadhili kuchochea na kupanga machafuko ya baada ya uchaguzi nchini Kenya mwaka 2007 na kusababisha zaidi ya watu elfu moja kupoteza maisha na maelfu kukimbia makwao.

Kesi ya naibu wake William Ruto na mwanahabari Joshua Arap Sang inaendelea kusikilizwa katika mahakama hiyo.